Event Date: 
14-07-2021

Siku ya Jumapili tarehe 11 Julai 2021 ilikuwa ni Siku ya Vijana katika Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront Cathedral, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka ili kutambua na kuthamini mchango wa vijana katika kulijenga na kuliendeleza neno la Bwana.

Katika siku hiyo muhimu kwa vijana na usharika kwa ujumla, vijana wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront walipata fursa ya kuongoza ibada zote tatu za siku hiyo zilizofuatiwa na tamasha la uimbaji. Akitoa neno la siku hiyo, Ndg Allen David ambaye pia ni mwimbaji wa Kwaya ya Agape, aliwaasa vijana kutokata tamaa bali waendelea kumtegemea Mungu katika nyakati zote wanazozipitia.

Kwaya ya Umoja wa Vijana ikiimba katika moja ya ibada za siku hiyo.

“Vijana inabidi tuendelee kuwa wavumilivu katika kutafuta mafanikio mbalimbali, kuwa mvumilivu katika kutafuta mchumba, kazi, elimu, pesa na mengine yanayofanana na hayo. Lakini unapobarikiwa ukapata mafanikio ukiwa kijana sio unaanza anasa bali unapaswa kuendelea kumtumikia Mungu,” alisema Ndg Allen.

Ndugu Allen aliwaasa vijana kuendelea kujitokeza na kushiriki katika shughuli na matukio mbalimbali ya usharika na kanisa kwa ujumla huku pia akiwasisitiza juu ya mambo muhimu ya kuzingatia kama kijana, aliyataja mambo hayo kama; uvumilivu pamoja na kuwaheshimu wazee, wazazi au walezi.

“Ndugu zangu vijana tujijengee utamaduni wa kujiweka mbele za Mungu kila wakati, njoo kanisani uombe hata kama sio siku ya Jumapili, kanisa liko wazi siku zote hivyo kila unapopata nafasi ni vyema kufika kanisani kufanya maombi,’’ alisema.

Ndg Allen David (kulia) ndiye alitoa neno la siku hiyo

Mbali na kuendesha ibada za siku nzima ya Jumapili, siku ya vijana iliendelea alasiri ambapo tamasha la uimbaji lilifanyika likizihusisha kwaya na vikundi vya burudani vya Umoja wa Vijana wa Usharika huku kwaya za vijana za sharika jirani pia zikialikwa kutumbuiza.

Akifungua tamasha hilo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Ndg Wilfred Moshi aliwataka vijana kutumia siku hiyo kumwabudu na kumsifu Mungu huku wakiweka mipango madhubuti juu ya namna ya kuuimarisha umoja wa vijana wa usharika kwa manufaa ya vijana wenyewe, usharika na kanisa kwa ujumla.

Neno na mafundisho katika siku ya vijana mwaka 2021 yalitoka katika kitabu cha 2 Timotheo 4: 1 -5 yakibebwa na kichwa cha neno kisemacho “Kijana Mkristo Katika Huduma Ya Misioni Na Uinjilisti"

Kwaya ya Umoja wa Vijana ikiimba katika moja ya ibada za siku hiyo.

Kikundi cha vijana wakisoma ngonjera mbele ya washarika katika ibada ya Tatu iliyofanyika siku hiyo.

Washarika wakiimba wimbo wa kuabudu katika ibada ya Tatu iliyofanyika siku hiyo Usharikani Azaniafront Cathedral.

Sehemu ya vijana na washarika wengine wakifuatilia ibada ya Tatu ilyofanyika Usharikani Azaaniafront Cathedral.

Kikundi cha vijana wakisoma ngonjera mbele ya washarika katika ibada ya Tatu iliyofanyika siku hiyo.

TAZAMA MATUKIO YOTE HAPA!

Ibada zote tatu pamoja na tamasha la siku hiyo vilirushwa moja kwa moja kupitia YouTube chaneli ya Azaniafront TV; kama ulikosa matukio yote ya siku hiyo unaweza kuyatazama kupitia link zifuatazo;

Ibada ya Kwanza - Kiswahili

Ibada ya Pili - English Service

Ibada ya Tatu - Kiswahili

Tamasha la Siku ya Vijana

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Ripoti hii imeandaliwa na: Paulin Paul