Date: 
02-07-2026
Reading: 
Luka 11:45-52

Alhamisi asubuhi 02.07.2026

Luka 11:45-52

45 Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi.

46 Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.

47 Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua.

48 Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara.

49 Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza,

50 ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu;

51 tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki.

52 Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.

Tumeitwa kutenda haki na huruma;

Yesu alikuwa amekaribishwa chakulani na Farisayo mmoja, akaketi mezani bila kunawa. Farisayo akastaajabu kwa sababu Yesu hakunawa mikono. Yesu akamwambia na wote waliokuwepo, kwamba wanasafisha nje ya kikombe, lakini mioyoni mwao kumejaa unyang'anyi na uovu. Yesu akaendelea kuwapa ole kadhaa, ikiwemo kupenda kukaa viti vya mbele, kusalimiwa njiani na kuacha mambo ya adili.

Somo la asubuhi hii linaanzia hapo, mmoja akimwambia Yesu kuwa anawashutumu wao. Yesu akaendelea kuwapa ole, kwamba wanabebesha wengine mizigo mizito na kuwaua manabii. Yesu anawataka Mafarisayo kumwamini yeye na kutenda yawapasayo, na siyo sheria. Tumwamini Yesu tukitenda haki na huruma kwa wenzetu. Amina

Siku njema

Heri Buberwa