Jumatano asubuhi tarehe 01.07.2026
Mithali 11:23-31
23 Haja ya mwenye haki ni mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu.
24 Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.
25 Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.
26 Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake.
27 Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia.
28 Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani.
29 Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili.
30 Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu.
31 Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?
Tumeitwa kutenda haki na huruma;
Mithali za leo zinahusu haki. Tunaanza kusoma kwanba haja ya mwenye haki ni mema tu, bali hitaji la mwovu ni ghadhabu. Aliye mtoaji kwa wengine kwa ukarimu hupokea baraka, atafutaye mema hupata fadhili, naye atafutaye madhara yatamjia. Mwandishi anaendelea kusema kwamba azitegemeaye mali zake ataanguka, naye mwenye haki atastawi kama jani.
Ukiangalia maudhui ya Mithali tulizonakili hapo juu ni haki, wema, huruma, upendo, hekima, ukarimu na mengine kama hayo. Ndiyo maisha tunayokumbushwa kuishi. Asubuhi ya leo tafakari wewe mwenyewe, kwamba nini nafasi yako katika kutenda haki? Wewe ni kielelezo cha kuwatendea wengine haki katika jamii inayokuzunguka? Usiache kutenda haki, hilo ni agizo toka kwa Mungu wetu. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
