Date: 
29-06-2026
Reading: 
Mwanzo 15:1-6

Jumatatu asubuhi tarehe 29.01.2026

Mwanzo 15:1-6

1 Baada ya mambo hayo neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.

2 Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski?

3 Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.

4 Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.

5 Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.

6 Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.

Tumeitwa kutenda haki na huruma;

Kabla hajabadilishwa jina na kuwa Ibrahimu (Mwa 17:5), Mungu anamtokea Abramu katika ndoto na kumwambia kuwa yeye (Mungu) ni ngao na thawabu kwake (Abramu). Abramu anamlalamikia Mungu kwa kutompa uzao ili apate mrithi. Bwana anamuahidi kumpa uzao ambao utakuwa mkubwa kwa mfano wa nyota za mbinguni.

Abramu anamuamini Bwana naye anahesabiwa haki ya kupata uzao. Tunachojifunza ni imani ya Abramu kumfanya ahesabiwe jambo la uzao kuwa haki kwake. Tukumbushane kwamba hatuwezi kujihesabia haki wenyewe, bali kwa imani katika Yesu Kristo kama Mtume Paulo alivyowaambia watu wa Rumi;

Warumi 3:22-24, 28

22 ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;
23 kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;
24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;
28 Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.

Mwamini Yesu Kristo, usiyumbe. Yeye ndiye mwenye kutuhesabia haki kwa neema yake. Haki hiyo hailipiwi, wala haitolewi sadaka kama baadhi wanavyofundisha siku hizi. Yesu alikufa, akafufuka, akapaa mbinguni. Kwa imani katika yeye, anatuhesabia haki, na siyo vinginevyo. Amina

Uwe na wiki njema

 

Heri Buberwa