
Siku ya Jumatano, 18 Februari 2026 ilifanyika ibada kuadhimisha Siku ya Jumatano ya Majivu katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front. Ibada hiyo iliongozwa na Mkuu wa Kanisa, Baba Askofu Dkt. Alex Malasusa na kuhudhuriwa na mamia ya washarika pamoja na wageni.
"Leo ni Jumatano ya kipekee sana katika maisha ya kiroho, ni Jumatano inayotuandaa kuingia katika kipindi cha toba, kipindi cha kutengeneza mbele ya Mungu. Ni Jumatano inayotukumbusha juu ya maisha yetu ya kiroho ya kila siku na ni kipindi cha kutafakari uhusiano wetu sisi na Mungu lakini pia uhusiano wetu na wanadamu wengine ambao Mungu amewaweka karibu nasi,"alisema Baba Askofu Malasusa wakati akifungua mahubiri ya siku hiyo.
Akizungumza katika Ibada hiyo Baba Askofu Malasusa alisema kuwa Kwaresma ni kipindi cha kujinyenyekeza na kutafakari juu ya matendo yetu (binadamu) kama yanaendana na kusudi la Mungu. "Kila mmoja anajua alivyomkosea Mungu. Mungu anatupa fursa hii sisi tuliofika katika ibada hii kuacha ibada za mazoea na kuingia katika toba ya kweli," alisema.
Aidha Baba Askofu alizungumzia juu ya umuhimu na namna ya kufunga (kutokula) akisema kwamba kufunga sio jambo la kutangaza bali ni jambo la siri kati ya mhusika na Mungu mwenyewe.
Katika hatua nyingine, Baba Askofu aliwapongeza washarika na wageni wote walioweza kuhudhuria ibada hiyo na kuwatakia baraka za Bwana katika kipindi cha Kwaresma.
Baadhi ya Matukio Katika Picha Kutoka Katika Ibada ya Jumatano ya Majivu. (Picha: AZ/ Media Team)

Tazama Ibada hiyo hapa chini
Ibada ya Jumatano ya Majivu: https://www.youtube.com/watch?v=6DMlHoB74UM
