Ijumaa asubuhi tarehe 14.11.2025
Luka 17:22-30
22 Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione.
23 Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate;
24 kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake.
25 Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki.
26 Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu.
27 Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote.
28 Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga;
29 lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote.
30 Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu.
Tuvumilie hata mwisho katika Bwana;
Yesu anaongea na wanafunzi wake kuhusu siku za mwisho, kwamba ipo siku watatamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu wasiione. Hapa aliongelea kuhusu kutamani kuwa na Yesu na kulisikia neno lake. Yesu anaongelea kufa kwake baada ya kuteswa kwa mateso mengi.
Yesu anafananisha siku hizo kama ilivyokuwa siku za Nuhu, kwamba watu walifurahi walivyotaka, hawakumsikiliza Nuhu alipowaambia kujenga safina. Gharika iliposhuka ikawaangamiza wote. Sodoma na Gomora vilevile, baada ya kustarehe waliangamia kwa moto. Kumbe tusikiapo neno la Mungu tusipuuze, ili Yesu akirudi asituache. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
