Date: 
25-10-2025
Reading: 
Maombolezo 3:22-24

Jumamosi asubuhi tarehe 25.10.2025

Maombolezo 3:22-24

22 Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.

23 Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu.

24 Bwana ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini yeye.

Imani Iletayo ushindi;

Nyimbo nyingi za Injili na baadhi ya nyimbo zitumikazo kwenye Liturjia hutumia mistari ya Biblia kama marejeo wakati wa kuimba, zikitoa ujumbe kwa wasikilizaji. Sehemu ya mistari katika somo la leo (mstari wa 22 na 23) ni mistari ijulikanayo sana. Mistari hii imetumika sana katika nyimbo mbalimbali. Ni sehemu ya nyimbo za huzuni na maumivu (uchungu). Ukweli ni kuwa mistari hii ni kiini cha kitabu cha Maombolezo.

Kitabu chenyewe;

Muundo wa kitabu cha Maombolezo huvutia. Ni sura tano zenye mashairi tofauti. Sura nne za kwanza zimeandikwa kwa mfuatano (accrosstic), ambapo sura ya 1, 2, na 4 zina mistari 22 kwa kuzingatia herufi 22 za Kihebrania. Mstari wa kwanza huanza na herufi ya kwanza, mstari wa pili herufi ya pili n.k Sura ya 3 ina mistari 66 kwa maana ya kila herufi inaanza kwa mistari mitatu. Sura ya tano, yaani ushairi wa tano siyo wa mfuatano (accrostic) lakini ina mistari 22! Hakika ni muundo unaoshangaza! Wasomi wa Agano la kale hawaonekani kujua lengo au kazi ya muundo wa uandishi wa kitabu hiki cha Maombolezo.

Fahamu;

Tunapoongelea mfuatano wa herufi (accrosstic) tunamaanisha herufi za kwanza kuonesha kitu fulani. Angalia mfano wa ushairi ufuatao;

 'H'aya tukalihubiri, neno lenye mausia

'E'limu ya umahiri, uzima kuelekea

'R'ejea hata shairi, wote wapate tubia

'I'mani yenye matendo, hutupeleka kwa Baba

Ukiangalia ushairi hapo juu, herufi za kwanza zinatengeneza neno "HERI". Sasa kwa kitabu cha Maombolezo, herufi za kwanza kwa mistari 22, hutengeza herufi 22 za Kihebrania. Nafikiri umenielewa sasa.

Mazingira ya kitabu kuandikwa;

Ashuru na Babeli zilikuwa katika Mesopotamia, eneo la mito ya Tigris na Efrata ilipo Iraq leo (650-800)km Kaskazini Mashariki mwa Israeli. Babeli (Mesopotamia kusini) iliishinda Ashuru (Mesopotamia kaskazini) na kuiweka chini yake. Mnamo 605 KK Mfalme Nebuchadnezzar wa pili wa Babeli aliishinda Misri akiweka himaya ya Babeli.

Mwaka 598 KK mfalme Nebuchadnezzar alifanya uasi katika Uyahudi kwa kuizingira Yerusalemu, akilazimisha raia wa Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli, na hazina yote ya nyumba ya Bwana (2Fal 24:13)

Mwaka 587 KK Mfalme Nebuchadnezzar alifanya uasi, kwa Mfalme Zedekia wa Uyahudi kwa kuizingira tena Yerusalemu. Mara hii aliuharibu mji na kuwaua wakazi wake wengi. Aliichukua Babeli yote iliyobaki, akiacha sehemu ndogo tu (2Fal 25). Wachache baadhi katika Yuda walifanya uasi hadi kumuua Gedalia, mtawala mwakilishi wa Babeli (2Fal 25:22-26), ikasababisha wao kuondoka Babeli. Manabii waliweka wazi kuwa ilikuwa hukumu ya Mungu kwa sababu ya dhambi.

Kitabu cha Maombolezo kiliandikwa wakati Israeli wakiwa uhamishoni Babeli, kati ya 587 KK na 539 KK pale Kairo wa Peresi alipowaachia mateka. 

Inaaminika kuwa sura nne za kwanza ziliandikwa wakati wa mwanzo uhamishoni. Sura ya tano iliandikwa baadaye, lakini uhamishoni huko huko. Kitabu chote ni kama Ombolezo kwa ajili ya Taifa. Maombolezo haya hayataji mwandishi, lakini uandishi wenyewe unasadikika ni wa Yeremia. Japokuwa kwa kulinganisha uandishi wa Maombolezo na Yeremia yenyewe, bado wasomi wa Agano la kale hugawanyika juu ya mwandishi wa Maombolezo. 

Katika maandiko ya Kihebrania, Maombolezo hupatikana katika maandiko ya kawaida tu, na siyo unabii. Ingawaje matoleo ya Kiyunani ya kale sana huyaweka Maombolezo baada ya kitabu cha Yeremia, na utaratibu wa uandishi wa kawaida ulifuata hilo hadi leo. 

Maudhui ya somo;

Yeremia analia, anaomboleza juu ya kuharibiwa kwa hekalu katika Yerusalemu kulikotokea mnamo 586 KK. Alilia kwa sababu watu waliweka imani yao na tumaini kupitia hekalu. Waliamini kuwa hekalu lingekuwepo kwa ajili yao. Alama ya Mungu ilikuwa hekalu. Waliweka alama moyoni mwao kuliko Mungu mwenyewe!

Kinachofahamika kuhusu Maombolezo ni kuwa ni mkusanyiko wa mashairi kuhusu kuharibiwa kwa Yerusalemu. Maombolezo hayasomeki kwa mwimbaji, bali anayahisi. Sasa kama msomaji, unaweza kuyaona maumivu ya Yeremia, akiumia kuipoteza ardhi ya asili. Sehemu aliyokuwa amekulia iliharibiwa! Marafiki zake wengi walikuwa wameuawa! Kila alichokifahamu na kukipenda kiliisha! Yeremia anaonesha maumivu yake;

Maombolezo 3:19-20

19 Kumbuka mateso yangu, na msiba wangu, Pakanga na nyongo.

20 Nafsi yangu ikali ikiyakumbuka hayo, Nayo imeinama ndani yangu.

Lakini bado Yeremia anaendelea kuwa na matumaini (21). Hii ni Imani ya wazi. Imani humweka aaminiye kwa Mungu wakati wote ikiwemo wakati wa shida. Maisha yakiwa rahisi huwa ni rahisi kuamini kuwa Mungu ni mwema na anaweza yote, lakini mambo yakienda mrama, maisha yakawa magumu, kuwa na tumaini katika Bwana huwa siyo rahisi. Hapa ndipo Imani ya kweli huonekana kwa kuwa na tumaini kuwa siku moja utapata msaada, uponyaji na na nafuu ya maumivu, utaacha kusumbuka n.k hiyo ndiyo imani, kama anayoionesha Yeremia.

Ni rahisi kusoma juu ya tumaini la Yeremia na imani yake kwa Mungu. Ni rahisi kuongelea imani kwa Mungu. Nadhani wengi wetu tunaamini katika msaada wa Bwana. Kigumu ni kuwa na imani katika mazingira magumu. Ni vigumu kuwa na imani, iwapo tumaini lenyewe linapotea. 

Matatizo ya kuharibiwa Yerusalemu yalianza taratibu, yalipozidi ndipo kwanza Yeremia akatunga na mashairi kabisa, akionesha kusimama na Bwana. Hapo kabla hakuwahi kukutana na mambo ya namna ile! Uvamizi, kupigwa, vifo, hekalu kuharibiwa, lakini bado anao udhubutu wa kutamka kuwa tumaini lake lipo kwa Bwana. Hali yako huwa inakuwaje pale unapokutana na hali ngumu ambayo hukuwahi kukutana nayo huko nyuma? Tumaini lako huwa linabaki kwa Bwana? 

Bila shaka hali ile ilimtisha Yeremia. Katika ubinadamu wake kuwa na tumaini lilikuwa jambo gumu sana. Hakuwa na makazi. Ndugu zake walikufa! Uhuru ulipotea. Lakini bado aliwaza na kuona tumaini lake lazima liwe katika Bwana. Unaweza kupoteza ndugu, makazi, nchi na bado ukaliita jina la Bwana?

 

Yeremia anaonesha uvumilivu katika Bwana, hivyo kutupa ujumbe wa Kumngojea Bwana. Kupitia maandiko, "kumngojea Bwana" ni kuishi katika Imani kwa kumtegemea, na kwamba rehema zake hazikomi. Kumngojea Bwana ni kuishi kwa kujua kuwa Bwana anayo nguvu na huwabariki wamwaminio. Kumngojea Bwana ni kuiona hali ya sasa kuwa nzuri baadaye kwa mkono wa Bwana, kama mfano wa ukombozi wa Israeli.

 

Tunapata funzo kuwa Bwana ni mwema kwa wote wamngojao. 

Israeli waliumia kwa kuvunjwa kwa hekalu, wakateseka uhamishoni. Lakini mstari wa 25 hadi 30 inaonesha imani katika Bwana. Mwandishi anaandika kuhusu imani, kwamba Mungu hataiadhibu Yuda milele, bali ataikomboa.

Imani Iletayo ushindi;

Kuharibiwa kwa hekalu hakukumuondolea imani Yeremia. Katika kuomboleza kwake anakiri kuwa Bwana angewaokoa Israeli. Ni kweli, baadaye walitoka uhamishoni. Mungu alionesha ukuu na upendo wake kwa kuwakomboa taifa lake. 

Mungu aliendelea kuonesha upendo wake kwa wanadamu, kwa kumtuma Yesu Kristo duniani, afe kwa ajili ya dhambi zetu. Leo katika dunia hii tuliyomo tunapitia mambo yaliyo mazuri, mengine magumu. Ni wakati wa kujifunza, kuwa tumtumie Yeremia kama Mwalimu wetu, kuwa katika shida zote tunazopitia, Mungu ni mwema, atatuwezesha kushinda, maana yeye ndiye hutuwezesha tangu mwanzo, sasa na siku zote. 

Mungu anapotulinda na kutupitisha katika nyakati ngumu siyo kwamba sisi ni wakamilifu, au tuko wasafi, au tunastahili, bali hutuwezesha bure. Kumbe tangu uumbaji, yeye hutuongoza na kutupa mahitaji yetu bure. Hii ni neema. Na kwa neema hii, tudumu katika imani kwake yeye ambaye ametuahidi uzima wa milele. 

Uwe na Jumamosi njema

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com