Event Date: 
28-09-2025

Siku ya Jumapili tarehe 28 Septemba 2025 katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front ilifanyika Sikukuu ya Mikaeli na Watoto; Sikukuu ambayo hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kumkumbuka Malaika Mikeli na watakatifu wote pamoja na watoto. Ibada hii hufanyika kwa kuongozwa na watoto wakisaidiana na walimu wao pamoja na watumishi wengine wa usharika (parish workers).

Kwa mwaka wa 2025, Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front zilifanyika ibada tatu kuadhimisha sikukuu hiyo, ibada za Kiswahili mbili na moja ya Kiingereza. Katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kuongoza shughuli zote za ibada ikiwemo kusoma litrugia, matangazo pamoja na kuongoza sala. Somo; Kumbukumbu la Torati 6: 6 - 9; Tuwapende na Kuwajali Watoto Katika Bwana.

Akihubiri katika ibada za Kiswahili, Mwalimu Laulah, aliwaasa washarika, wazazi pamoja na walezi kuhakikisha wanawalea watoto katika njia zinazompendeza Mungu nyakati zote. “Imani huanzia nyumbani,wazazi au walezi ndio shule ya kwanza ya imani. Watoto wanajifunza kuhusu Mungu kwanza kutoka kwa Wazazi au Walezi na sio kanisani au shule ya Jumapili”, alisema. 

Mwalimu Laulah pia aliwaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa mfano bora kwa watoto wao na kwamba suala la kumfundisha mtoto maadili mema ya kikristo sio jambo la siku moja bali ni endelevu. “Imani ni kwa mfano hai, watoto hawajifunzi kwa kuambiwa bali wanajifunza kwa kuona na kuishi hivyo. Siwezi kumwambia mwanangu usiseme uongo lakini ananisikia nimeongea na simu nikisema nipo Posta wakati nipo nyumbani. Kulea sio somo moja la imani bali ni mtindo wa maisha,” aliongeza.

Pia katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kusema mistari ya moyo, kufanya ngonjera na kuimba nyimbo mbalimbali. Vyote hivyo vilibeba ujumbe kwa wazazi kuhusu kuwalea watoto vyema ili wakue katika maadili mema ya kikristo.

Kwa upande wake, Parish Worker wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front, kwa niaba ya Mchungaji Kiongozi wa Usharika Chaplain Charles Mzinga, aliwashukuru walimu, wazazi, walezi na washarika wote kwa ujumla kwa kufanikisha Sikukuu ya Mikaeli na watoto kufanyika kwa mafanikio makubwa.

Mapema siku ya Jumamosi tarehe 27 Septemba 2025, watoto walikusanyika katika viwanja vya Usharika ambapo walipata fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo kuonyesha vipaji vyao; kuchora, kuimba, kucheza pamoja na kushiriki keki ya pamoja.

Picha zaidi, zipo hapa chini. 

Matukio mbalimbali katika picha wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mikaeli na Watoto yaliyofanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral, tarehe 27-28 Sept 2025. Picha: AZF Media Team.