Date:
13-10-2025
Reading:
Luka 6:1-5
Jumatatu asubuhi tarehe 13.10.2025
Luka 6:1-5
1 Ikawa siku ya sabato moja alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke na kuyala, wakiyapukusa-pukusa mikononi mwao.
2 Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato?
3 Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao?
4 Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao.
5 Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
Kristo ametuweka huru;
Mafarisayo walichukizwa na wanafunzi wa Yesu kupita mashambani wakivunja masuke na kuyala siku ya sabato. Wakamuuliza Yesu kwa nini wanafunzi walifanya vile isivyo halali siku ya sabato? Yesu akawajibu kwa kuwarejesha kwenye historia jinsi ambavyo Daudi aliumwa na njaa akaingia hekaluni na kula mikate, tena akawapa na wenzake wakati mikate ilikuwa halali kuliwa na makuhani pekee!
Mafarisayo walikuwa na mawazo ya sabato ya Kiyahudi, ile ya Agano la kale. Lakini katika somo Yesu anahitimisha kwamba yeye ndiye Bwana wa sabato. Yesu alikuwa anawaambia Mafarisayo kwamba yeye yuko juu ya hiyo sabato yao, hivyo walitakiwa kumwamini yeye. Yesu huyu ndiye ametuweka huru, hatuko chini ya sabato bali Kristo. Kwa kutuweka huru, anatuita kumwamini yeye pekee daima. Amina
Tunakutakia wiki njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650