Jumatano asubuhi tarehe 08.10.2025
Matendo ya Mitume 16:35-40
35 Kulipopambauka makadhi wakawatuma wakubwa wa askari wakisema, Waacheni watu wale waende zao.
36 Yule mlinzi wa gereza akamwarifu Paulo maneno haya akisema, Makadhi wametuma watu ili mfunguliwe; basi, sasa tokeni nje, enendeni zenu kwa amani.
37 Paulo akawaambia, Wametupiga mbele ya watu wote bila kutuhukumu, na sisi tu Warumi, tena wametutupa gerezani; na sasa wanataka kututoa kwa siri? Sivyo, lakini na waje wenyewe wakatutoe.
38 Wakubwa wa askari wakawapasha makadhi habari za maneno haya; nao wakaogopa, waliposikia ya kwamba hao ni Warumi.
39 Wakaja wakawasihi; na walipokwisha kuwatoa nje, wakawaomba watoke katika mji ule.
40 Nao wakatoka gerezani wakaingia nyumbani mwa Lidia; na walipokwisha kuonana na ndugu wakawafariji, wakaenda zao.
Mungu hututunza kwa uwezo wake mkuu;
Paulo alimuombea kijakazi mmoja pepo akamtoka. Kijakazi huyu alikuwa akiwapatia waajiri wake fedha nyingi kwa sababu ya uaguzi. Basi waajiri wa yule kijakazi wakakasirika. Paulo akakamatwa akiwa na Sila, wakawashtaki, wakavuliwa nguo, wakachapwa bakora na kutupwa gerezani. Wakiwa huko gerezani walimsifu Mungu, gereza likafunguka wakatoka. Askari mlinzi aliyeshuhudia gereza likifunguka usiku aliogopa akataka kujiua. Paulo akamzuia asijiue, yule askari akaamini na kubatizwa, usiku uleule na familia yake yote.
Somo letu linaanzia hapo, ni asubuhi, wakubwa walipopata habari zao jinsi gereza lilivyofunguka usiku wakatuma ujumbe kuamuru waondoke. Paulo akawataka waje wawatoe, maana waliwakamata wenyewe. Wakubwa waliposikia ni Warumi wakaogopa, wakawaomba waondoke. Tunachojifunza asubuhi ya leo ni kuwa Paulo na Sila waliendelea kutunzwa na Mungu katika utume wao hata gerezani, wangehubiri kwa akili zao wasingeweza. Nasi kwa akili zetu hatuwezi lolote, bali Mungu ndiye hututunza kwa uwezo wake mkuu. Amina
Jumatano njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650