Jumatatu asubuhi tarehe 06.10.2025
Luka 7:11-17
11 Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa.
12 Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.
13 Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie.
14 Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka.
15 Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake.
16 Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.
17 Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.
Mungu hututunza kwa uwezo wake mkuu;
Tunalianza juma jipya kwa kusoma habari ya Yesu kumfufua kijana mmoja katika mji wa Naini. Kijana huyu alikuwa ni mtoto wa pekee kwa mama yake. Hapa unaweza kuona ni maumivu ya kiwango gani alikuwa nayo mama huyu kwa kufiwa na kijana wake wa pekee. Biblia haisemi kama kijana aliugua kwa muda mrefu au mfupi, alipata ajali n.k taarifa iliyopo ni kwamba alifariki na alikuwa anaenda kuzikwa. Tunaona Yesu akimwonea huruma yule mama na kuligusa jeneza, akamwambia kijana inuka, kijana akainuka na kuanza kusema. Hofu ilitanda, habari hii ikaenea ndani ya Uyahudi wote na nchi zote za jirani.
Tunachoona asubuhi ya leo ni huruma ya Yesu kwa yule mama aliyekuwa amefiwa na mtoto wa pekee. Furaha ya mama ilirudi palepale baada ya mtoto wake kuinuka tena na kuwa mzima. Bila shaka hakuishi milele, ila lengo la ujumbe huu ni kuonesha huruma ya Mungu kwa watu wake, kwamba katika hali zote huwashika watu wake. Basi na tumwamini yeye ambaye hututunza kwa uwezo wake mkuu. Amina
Uwe na wiki njema ukitunzwa na Mungu.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650