Jumamosi asubuhi tarehe 20.09.2025
Warumi 14:1-6
1 Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake.
2 Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga.
3 Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali.
4 Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.
5 Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.
6 Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu.
Mtendee mema jirani yako;
Mtume Paulo anawaandikia Warumi akiwataka kutowahukumu wengine, badala yake kushirikishana mawazo na kusaidiana ili kila mmoja asonge mbele katika safari ya Imani. Paulo anashauri kumkaribisha aliye dhaifu wa imani, na siyo kumhukumu mawazo yake. Paulo anahoji uhalali wa mtu mmoja kumhukumu mwingine, anasema sote tu watumishi wa Bwana, hivyo katika Bwana huyo wote wapendane na siyo kuhukumiana.
Asubuhi hii kila mmoja ajiulize swali hili la Paulo; mimi ni nani kumhukumu mwingine? Paulo anatukumbusha kutonyoosheana vidole na kuhukumiana, bali kupendana, kushauriana, kuelekezana na kukaribishana. Ni kwa njia hii tunakuwa kundi moja la waaminio, yaani Kanisa moja chini ya Mchungaji mkuu Yesu Kristo. Basi tutendeane mema kwa utukufu wa Mungu. Amina
Jumamosi njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650