Ijumaa asubuhi tarehe 19.09.2025
Luka 6:39-42
39 Akawaambia mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili?
40 Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake.
41 Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii?
42 Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.
Mtendee mema jirani yako;
Leo asubuhi tunasoma Yesu akifundisha juu ya watu kupendana, kila mmoja kumjali na kumheshimu mwenzake. Katika somo tulilosoma, Yesu anasema kipofu hawezi kumuongoza kipofu, mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake! Hapa Yesu alikuwa anaonesha kwamba tunategemeana, na kwa njia hiyo jambo la muhimu ni kupendana na kuheshimiana.
Mstari wa 41 unaonya juu ya kutazama kibanzi kwenye jicho la ndugu, wakati mwenyewe una boriti kwenye jicho lako! Yesu anasema kumuona mwenzako kwamba ana kibanzi kwenye jicho wakati wewe una boriti ni unafiki! Toa kwanza boriti kwenye jicho lako ndipo umsaidie mwenzako kutoa kibanzi! Hata wewe ni mwenye dhambi kama mtu mwingine yeyote alivyo, sote tunaishi kwa neema ya Mungu. Tuache kunyooshea watu vidole kama vile sisi ni watakatifu kuliko wengine. Tuishi kwa kutendeana wema, na siyo unafiki! Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650