Date: 
28-07-2025
Reading: 
Waefeso 5:1-2

Jumatatu asubuhi tarehe 28.07.2025

Waefeso 5:1-2

1 Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa;

2 mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.

Mambo yote yatendeke katika upendo wa Kristo;

Mtume Paulo anawaandikia waefeso akiwaelekeza jinsi ya kuishi maisha mapya. Ukisoma kabla ya somo la leo asubuhi unaona mtume Paulo akiwaelekeza watu wa Efeso kuishi kwa kuhurumiana na kusameheana wao kwa wao;

Waefeso 4:31-32

31 Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;
32 tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

Kwa kuenenda hivyo, ndipo Paulo anawasihi watu wa Efeso kumfuata Mungu kwa upendo, kwa mfano wa Kristo mwenyewe. Paulo anatoa mfano wa Yesu alivyokufa msalabani kwa ajili ya Kanisa lake, yaani upendo wa Kristo kwa watu wake. Maisha ya waaminio ni ya kupendana kama lilivyo agizo la Kristo. Tupendane. Amina

Tunakutakia wiki njema yenye Upendo.

 

Heri Buberwa