Jumatatu asubuhi tarehe 30.06.2025
Mwanzo 15:1-6
1 Baada ya mambo hayo neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.
2 Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski?
3 Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.
4 Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.
5 Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.
6 Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.
Wito wa kuingia Ufalme wa Mungu;
Baada ya Abram (baadaye Abraham) kuwa ametii agizo la Bwana na kuhama nchi ya baba zake kwenda nchi nyingine, asubuhi hii tunasoma akimuomba Mungu kumpa uzao maana hakuwa na mtu wa kumrithi. Bwana anamwambia kuwa yeye ni ngao yake na thawabu yake (1). Lakini Bwana anamuahidi Abram uzao mkubwa sana, akimuonesha mbingu kwamba azihesabu nyota maana ndivyo utakavyokuwa uzao wake.
Ahadi hii kwa Abram ilikuwa ya kweli, maana alikuja kuwa na uzao mkubwa sana. Ahadi ya Mungu kwetu leo iliyo kuu kuliko zote ni wokovu kwa neema yake. Kwa ahadi hiyo tunakumbushwa kudumu katika imani kama tulivyompokea Yesu pale tulipoamini na kubatizwa. Tunaitwa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa kusimama katika imani yetu daima, na Bwana hatatuacha. Amina
Uwe na wiki njema
Heri Buberwa