Date: 
10-06-2025
Reading: 
Matendo ya Mitume 13:49-52

Jumanne asubuhi tarehe 10.06.2025

Matendo ya Mitume 13:49-52

49 Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote.

50 Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao.

51 Nao wakawakung'utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio.

52 Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu ni ushindi wetu;

Paulo akiwa na Barnaba na wenzake waliingia Antiokia, mji wa Pisidia. Ilipofika Sabato wakaenda kwenye Sinagogi. Baada ya kusomwa torati na chuo cha manabii, Mitume wakapewa nafasi kusema neno. Paulo akaitumia fursa hiyo sawasawa kuhubiri Injili. Alisimulia ukombozi wa Taifa la Mungu tangu Agano la kale, hadi Wayahudi walivyomsulibisha Yesu, hadi kufufuka kwake na kupaa mbinguni. Akahitimisha kwa kusema kuwa huyo waliyemkataa ndiye Mwokozi wa Ulimwengu.

Wapo wengi walioamini kupitia Injili ya Paulo kwenye Sinagogi, lakini wapo Wayahudi ambao hawakuamini kabisa. Ndiyo kwanza wakaanza kuwatukana Mitume wakikanusha mahubiri yao yote.

Ndipo somo linasema kuwa Injili ikaenea katika nchi yote ile. Wayahudi wakawafanyia fujo mitume, lakini wao (mitume) wakaondoka kuelekea Ikonio. Mstari wa 52 unahitimisha kuwa wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu 

Ni wazi kwamba Mitume walijawa na Roho Mtakatifu katika kazi yao. Roho huyu ndiye aliyewaongoza kuhubiri Injili kwa ujasiri mbele ya Wayahudi ambao hawakutaka kusikia habari za Yesu. 

Mitume waliweza kuhubiri kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Nasi tunaweza kufanya yote kwa msaada wa Roho Mtakatifu, Mungu mwenyewe. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa 

Mlutheri