Date:
03-06-2025
Reading:
Yakobo 5:16-18
Jumanne asubuhi tarehe 03.06.2025
Yakobo 5:16-18
16 Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.
17 Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.
18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.
Mungu husikia maombi yetu;
Somo la leo asubuhi ni mwendelezo wa somo la mahubiri ya Jumapili iliyopita, ambapo Yakobo anaandika akihimiza yapasayo kwenye kuomba, tukizingatia toba, msamaha, na Upendo miongozi mwetu tukiombeana.
Yakobo anatufundisha nini?
1.Tuwe watu wa toba na msamaha
Yakobo anatukumbusha kusamehe wenzetu wanaotukosea, ili Mungu apokee sala zetu. Jaribu kutafakari, yaani wewe hujamsamehe mwenzako, halafu unaomba kusamehewa! Yaani wewe kusamehe hutaki ila unataka kusamehewa!
Kabla hujapeleka sala yako kwa Mungu, hakikisha umesamehe.
2.Yakobo pia anatukumbusha kuombeana.
Kuombeana ni tafsiri ya Upendo uliokomaa. Yaani tukipendana, tunaombeana, na Kanisa la Kristo linazidi kusimama
Tupendane, tuombeane.
3.Yakobo anatukumbusha pia kuishi maisha ya haki.
Maisha ya haki ni pale tunapoishi maisha ya uchaji, tukizingatia Mungu anachukia dhambi. Tunawajibika kutenda mema kadri tulivyoagizwa, ili Mungu apokee sala zetu.
Mungu ni mwema kwa wote, ila sisi tulioijua kweli lazima tuishi kwa kutenda mema, ili tunapopeleka haja zetu kwa Mungu, tuwe wenye haki.
Asubuhi ya leo tunakumbushwa kuomba, na tujue kuwa tunapoomba tunaongea na Mungu wetu. Pia tumuombe Mungu wetu peke yake, ndio maana tunakumbushwa kuomba, kwa uhakika kuwa Mungu anasikia kuomba kwetu. Amina
Siku njema
Heri Buberwa