Hii ni Pasaka;
Jumanne asubuhi tarehe 20.05.2025
Ezra 3:10-13
10 Hata wajenzi walipouweka msingi wa hekalu la Bwana, wakawaweka makuhani, wamevaa mavazi yao, wenye baragumu, na Walawi, wana wa Asafu, wenye matoazi, ili wamhimidi Bwana, kama alivyoagiza Daudi, mfalme wa Israeli.
11 Wakaimbiana, wakimhimidi Bwana, na kumshukuru, wakasema, Kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake kwa Israeli ni za milele. Kisha watu wote wakapaza sauti zao, na kupiga kelele, walipomhimidi Bwana, kwa sababu msingi wa nyumba ya Bwana umekwisha kuwekwa.
12 Bali makuhani wengi, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa, waliokuwa wameiona nyumba ya kwanza, wakati msingi wa nyumba hii ulipowekwa mbele ya macho yao, walilia kwa sauti kuu; na watu wengi walipiga kelele za furaha;
13 hata watu wasiweze kupambanua kelele za furaha, na kelele za vilio vya watu; maana watu walipiga kelele kwa sauti kuu, na kelele zao zikasikilikana mbali sana.
Kila mwenye pumzi amsifu Bwana;
Sura ya tatu ya Ezra inaangazia juu ya wana wa Israeli kurudi toka uhamishoni, hasa azma yao ya kujenga upya maisha yao ya kiimani na hekalu ndani ya Yerusalemu. Walijenga madhabahu, wakatoa sadaka, walisherehekea sikukuu ya vibanda, wakionesha utayari wao wa kumwabudu Bwana katika kurejea kwao. Waliweka msingi wa hekalu jipya, tukio ambalo lilikuwa na furaha sana. Sehemu ya kwanza ya sura ya tatu ni ibada kurejeshwa Yerusalemu, na sehemu ya pili ni kuwekwa msingi wa hekalu.
Sehemu ya pili ndiyo somo la asubuhi hii, ambapo Israeli wanaweka msingi wa hekalu na kumwabudu Bwana kama alivyoagiza Daudi. Walimsifu Bwana wakisema fadhili zake ni za milele. Walipiga kelele kwa sauti kuu, kwa jinsi walivyomshangilia Bwana. Ni ukumbusho kwetu, kwamba tulivyo ni kwa neema ya Mungu, hivyo tumpe sifa na tukuzo kwa kuishi tukitenda yatupasayo. Amina
Jumanne njema
Heri Buberwa