Hii ni Pasaka
Ijumaa asubuhi tarehe 16.05.2025
Marko 8:34-38
34 Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.
35 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.
36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
37 Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?
38 Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.
Ndani ya Yesu kuna maisha mapya;
Somo la asubuhi ya leo ni mwendelezo wa Yesu alipokuwa akitoa taarifa ya kufa kwake. Ukianzia mstari wa 31 Yesu anawaambia kuwa imempasa kupata mateso mengi, kukataliwa na wazee, wakuu wa makuhani, waandishi, kuuawa na kufufuka siku ya tatu. Yesu alikuwa akiwaandaa wanafunzi kuishi bila yeye baada ya kumaliza kazi yake na kuondoka.
Kwa muktadha huo, Yesu anawaambia kujikana na kujitwika msalaba, yaani kuishi kwa njia ya neno lake kwa kutenda yapasayo. Anawaita kujitoa nafsi zao kwa ajili yake, maana yeye ndiye mwenye hatma yao. Tunaalikwa kujikana na kujitwika msalaba, yaani kudumu katika imani, ili maisha yetu yawe mapya daima katika Kristo. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa