Hii ni Pasaka
Jumatano asubuhi tarehe 14.05.2025
Yohana 17:4-10
4 Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.
5 Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.
6 Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika.
7 Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako.
8 Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.
9 Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako;
10 na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao.
Ndani ya Yesu kuna maisha mapya;
Sura ya 17 ya Injili ya Yohana ni sala, ambayo ni hitimisho la mafundisho yake katika sura ya 14 hadi 16. Ni baada ya sala hii alikamatwa na kusulibiwa. Ni maoni yangu kuwa, sala hii ambayo ni sala ndefu ya Bwana Yesu iliyoandikwa miongoni mwa sala alizosali, ililengwa kusikika na wanafunzi wake, moja ya lengo likiwa ni kuleta faraja na tumaini kwa mioyo ya wanafunzi iliyovunjika.
Tukirejea somo la asubuhi hii ambalo ni sehemu ya sala hiyo, tunaona ilikuwa si kwa ajili ya wanafunzi tu, bali kwa Kanisa lote. Yesu anamtukuza Baba yake, kwa ajili ya Kanisa lake. Anawaweka watu wote kwa Baba yake, na wote ni wa kwake. Yaani sisi wote ni wa Kristo, hivyo tumtumaini yeye daima ili maisha yetu yawe mapya siku zote. Amina
Jumatano njema
Heri Buberwa