Date: 
13-05-2025
Reading: 
Hosea 2:14-23

Hii ni Pasaka;

Jumanne asubuhi tarehe 13.05.2025

Hosea 2:14-23

14 Kwa hiyo angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo.

15 Nami nitampa mashamba yake ya mizabibu toka huko, na bonde la Akori kuwa mlango wa tumaini; naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri.

16 Tena siku hiyo itakuwa, asema Bwana, utaniita Ishi

17 Kwa maana nitayaondoa majina ya Mabaali kinywani mwake, wala hawatatajwa tena kwa majina yao.

18 Nami siku hiyo nitafanya agano na wanyama wa mashamba kwa ajili yao, tena na ndege wa angani, tena na wadudu wa nchi; nami nitavivunja upinde na upanga na silaha vitoke katika nchi, nami nitawalalisha salama salimini.

19 Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema.

20 Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua Bwana.

21 Tena itakuwa siku hiyo, mimi nitaitika, asema Bwana; nitaziitikia mbingu, nazo zitaiitikia nchi;

22 nayo nchi itaiitikia nafaka na divai na mafuta; nayo yataiitikia Yezreeli.

23 Nami nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitamrehemu yeye asiyepewa rehema; nami nitawaambia wale wasiokuwa watu wangu, Ninyi ndinyi watu wangu; nao watasema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

Ndani ya Yesu kuna maisha mapya;

Sura ya pili ya Nabii Hosea inaongelea hukumu kwa Israeli kwa kukosa imani kwa Mungu, hali inayoandikwa kama uzinzi. Tangazo la hukumu linakuja na taarifa ya urejesho na upatanisho. Hosea anaonesha sura ya Mungu kama mume aliyevunjika moyo, ambaye mke wake amegeukia miungu mingine, lakini akitaka kumrudisha. Lugha ya mume na mke inatumika, lakini ujumbe ukiwa kwa Israeli kumrudia Mungu aliyewakomboa. 

Tukiwa bado katika majira ya Pasaka, tukumbuke kuwa ndani ya Yesu mfufuka ndipo kuna maisha mapya. Maisha mapya ni pale tunapoishi na Kristo daima, yaani Yesu akiwa kiongozi wetu katika mambo yote. Tumeona Israeli wakitangaziwa hukumu kwa kutoamini. Nasi tusipoamini hukumu yaja. Tukikaa kwa Yesu maisha yetu yanakuwa mapya daima, na tutakuwa na mwisho mwema. Amina

Jumanne njema

 

Heri Buberwa