Date: 
08-05-2025
Reading: 
Mathayo 9:35-38

Hii ni Pasaka

Alhamisi asubuhi tarehe 08.05.2025

Mathayo 9:35-38

35 Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.

36 Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.

37 Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.

38 Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.

Yesu ni Mchungaji mwema;

Baada ya hotuba ya mlimani (Mt sura ya 5-7) Yesu anaendelea na huduma yake kuanzia sura ya 8 ambayo pamoja na mafundisho iliambatana na ishara mbalimbali. 

Tunaona katika somo asubuhi hii, makutano waliomfuata Yesu hadi wakaonekana kuchoka, hadi Yesu akawahurumia maana aliwaona kama kondoo wasio na Mchungaji.

Asubuhi hii tujifunze;

1.Makutano walimfuata Yesu kwa muda mrefu. Hawa wanatupa picha ya kukaa miguuni pa Yesu wakati wote. Wanatufundisha maisha ya kudumu katika Imani, ambayo ni ya kuishi kwa kadri ya mapenzi ya Mungu. Nini nafasi yako katika hilo?

2.Yesu anawahurumia makutano, ambao wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na Mchungaji. Huruma hii ndiyo inamtambulisha Yesu kama Mchungaji mwema. Kumbe Yesu ndiye Mchungaji wetu mwenye huruma. Anatuita kumwendea katika nyakati zote, ili atuchunge yeye. Wajibu wetu ni kuitika na kubaki zizini. 

3.Mungu anatutuma kuifanya kazi yake tukiwaleta watu kwake. Ndio maana anasema mavuno ni mengi lakini watendakazi wachache. Sisi ndiyo watendakazi tunaoitwa kuwaleta kondoo wenzetu zizini. Unatimiza wajibu wako katika hili?

Nakutakia Alhamisi njema.

 

Heri Buberwa