Hii ni Pasaka
Jumatano asubuhi tarehe 07.05.2025
Matendo ya Mitume 20:32-35
[32]Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa.
[33]Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu.
[34]Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami.
[35]Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.
Yesu ni Mchungaji mwema;
Mtume Paulo anaagana na wazee wa Efeso waliokutana naye Mileto akiwa njiani kuelekea Yerusalemu. Akifunuliwa na Roho Mtakatifu, Mtume Paulo alifikiri huenda ilikuwa mara ya mwisho kukutana na hawa ndugu. Kwa nini nasema hivi?
Hebu soma hapa;
Matendo ya Mitume 20:25
[25]Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena.Ukisoma kuanzia mstari wa 23, unaona bila shaka kuwa mashtaka na kifungo vilimsubiri Mtume Paulo kama alivyokuwa amezoea katika kuhubiri Injili ya Kristo akiwa na wenzake. Baada ya miaka ishirini ya huduma Wayahudi wakimtafuta, kifo kilikuwa hakiepukiki kwake maana alianza kuingia katika moyo wa Uyahudi, yaani Yerusalemu yenyewe. Katika hotuba ya kuagana ndipo anawakumbusha Yesu alivyohimiza kutoa kuliko kupokea.
Nukuu ya "ni heri kutoa kuliko kupokea" katika somo letu inaonekana ni Mtume Paulo akimnukuu Yesu Kristo. Lakini nukuu hii haijaandikwa kwenye Injili yoyote. Paulo alikuwa anaikumbuka mwenyewe, labda kutoka kwenye mahubiri ya Petro au kutoka kwa mmoja wa mitume wengineo, au huenda aliisikia kutoka kwa Yesu mwenyewe aliyemtokea huko Arabia;
Wagalatia 1:17
[17]wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski.Nukuu hii ni muhimu sana, kiasi kwamba imenukuliwa kwenye waraka kwanza wa Clement (1 Clement 2:1). Hapa Clement anamnukuu Paulo moja kwa moja kwenye somo la leo (20:35) na hii inafanya nukuu hii kuwa ya kwanza kunukuliwa nje ya maandiko (Waraka wa Clement ni miongoni mwa apocryphal books).
Sasa kama waandishi kadhaa, tena mitume walikwenda na nukuu hii, waliona umuhimu wake. Kumbe na sisi inatuhusu, kwamba "ni heri kutoa kuliko kupokea"
Mtume Paulo anaonesha kuwa kama unapokea, basi iko haja ya kutoa. Asili ya kutoa ni upendo, na asili ya upendo ni Mungu wetu aliyetupenda akamtuma Yesu afe kwa ajili yetu. Upendo wa Mungu ni wa pekee na tofauti, maana hutoka kwake kuja kwa wote! Mtume Paulo alikuwa shuhuda wa upendo wa Mungu kwa jinsi alivyookolewa na kuacha kulitesa Kanisa, akaanza kutoa alichopewa kwa ajili ya watu wa Mungu. Ni kwa njia hii anakazia leo kuwasaidia walio wanyonge akikumbuka maneno ya Yesu, kwamba "ni heri kutoa kuliko kupokea".
Mtazamo wa Paulo katika kazi ya kuhubiri ilikuwa ni ujumbe wake kupokelewa kama zawadi itokayo kwa Kristo. Paulo alijua kuwa mhubiri lazima atunzwe madhabahuni;
1 Wakorintho 9:14
[14]Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.Lakini Paulo hakufanya hivyo, yaani hakutaka kutunzwa na aliowapelekea habari njema akiwa na Barnaba;
1 Wakorintho 9:12
[12]Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo.Paulo ameandika mahali pengine;
1 Wathesalonike 2:9
[9]Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu.Simaanishi Kanisa lisiwatunze watumishi wa Mungu, huo ni wajibu wetu. Naelezea tu mazingira ya Paulo. Yeye alikuwa Mtume aliyesafiri sehemu moja hadi nyingine kuhubiri kama alivyotumwa (mitume wa siku hizi wana ofisi, wametumwa hapo hapo walipo)
Paulo alitaka watu waangalie baraka walizopata toka kwa Mwenyezi Mungu kuanzia kwa msamaha wa dhambi, neema, na mali kwa ujumla halafu wawajali wengine. Ndipo leo anamnukuu Yesu akisema "ni heri kutoa kuliko kupokea".
Kutoa huanzia moyoni. Kama hujapenda huwezi kutoa kutoka moyoni. Mungu alitupenda akamtoa Yesu. Huo ni mfano tosha. Kumbe tukimpenda Mungu tunamtolea kwa moyo! Na kwa ndugu zetu vivyo hivyo. Mtume Paulo analialika Kanisa kutoa kwa njia ya vipawa ambavyo hutoka kwa Mungu. Katika kutoa huko, anaonesha kuwa kupenda fedha ni mhimili wa uovu;
1 Timotheo 6:10
[10]Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.Hapa fedha inasimama ikiwakilisha mali tulizo nazo. Lakini kwa upana wake, karama tulizopewa pia. Tunatoa inavyostahili?
Au tukishapokea tunatulia?
Kila mmoja anayo baraka ya neema, msamaha wa dhambi na uzima wa milele katika Yesu Kristo (mst 32) bure.
Lakini pia, kupenda fedha kunaweza kuwa kizuizi kwa Injili ya kweli pale wahubirio wanapolenga fedha. Mafundisho hutisha watu watoe, na siyo kumtolea Mungu kwa moyo. Ni muhimu kufundisha waumini wamtolee Mungu kwa moyo, na kusaidiana kama lilivyo agizo takatifu la Mungu.
Tuweke mazingira ya kutoa kwa ajili ya kazi ya Mungu kwa msingi wa neno la Mungu. Yaani watu waijue neema ya Mungu na wamtolee kwa upendo, imani na shukrani. Mtume Paulo alikuwa mfano katika hili, maana yeye alichagua kutengeneza mahema na kutoa Injili bure;
Matendo ya Mitume 18:3
[3]na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema.Maana yake nini?
Watu wamtolee Mungu kwa kuamini na kumjua wanayemtolea, pasipo vitisho. Wakiifahamu neema yake, watajua kuwa "ni heri kutoa kuliko kupokea". Paulo alitengeneza mahema kuonesha kuwa matoleo siyo kwa ajili yake, bali kwa ajili ya Mungu ili kazi yake ifanyike. Kumbe tunalo jukumu la kuwafundisha watu kuwa kazi ya kuipeleka Injili ni yetu, na kwa neema ya Bwana tuliyopewa, "ni heri kutoa kuliko kupokea" .
Katika kutoa huku, Mtume Paulo anatuasa kuwasaidia wanyonge. Wanyonge hapa ni tafsiri pana. Hawa ni ndugu zetu wanaoteseka dhambini. Hawajamjua Kristo. Hawa ni wale wanaoona madhara ya dhambi kwa kuumia, kuumwa, majanga na majaribu mbalimbali. Katika Imani, ni wale walio na ibada ya sanamu bado. Wenye ubinafsi na tamaa. Mimi na wewe ni wanyonge tunaohitaji neema ya Mungu na baraka, ambapo upendo unaweza kutupa njia sahihi. Mungu anatupa msamaha wa dhambi, uzima wa milele na maisha ya uhuru kwa njia ya Roho Mtakatifu kila siku kwa sababu ya Yesu Kristo aliyetuokoa. Hivyo kwa neema hii, hatuwezi kukwepa "kutoa".
Tunapomtolea Mungu hatuhitaji kujisikia kulazimishwa, au kutegemea malipo (something in return). Kutegemea matokeo baada ya kutoa huo siyo utoaji! (Kuna shida kubwa hapa siku hizi). Kuambiwa toa ili Mungu akupe hiyo ni "business deal". Sisi tumepewa vitu vyote muhimu na Mungu katika maisha yetu. Mungu ametupa nguvu ya kufanya kazi, na kwa matokeo yetu kumtolea kwa moyo. Yesu ametupa bure, hivyo tutoe bure;
Mathayo 10:8
[8]Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.Tusitegemee pongezi, wala tusisubiri hamasa kutoa. Vitu vyote ni vyetu kama mawakili, tumepewa na Bwana, tuvitunze na kuvitoa kwa ajili ya kazi yake;
1 Wakorintho 3:22-23
[22]kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; [23]nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.
Mwisho;
Tumeona Mtume Paulo akiagana na wazee wa Efeso, ujumbe wake ukiwa ni kuwakumbusha neema waliyoipokea kutoka kwa Kristo, na kuifanya kazi ya kuhubiri Injili bila masharti kwa kundi la waaminio.
Ujumbe huu unatujia leo kutukumbusha neema ya Mungu kwetu, ambayo kwa hiyo tunapata msamaha wa dhambi na uzima wa milele. Tunaalikwa kuwasaidia wanyonge kwa karama na mali zetu, tukikumbuka maneno ya Yesu kuwa "ni heri kutoa kuliko kupokea". Hii ni nafasi tuliyopewa katika utume huu, yaani kumtolea Bwana kwa ajili ya kazi yake. Tusiipoteze neema hii katika ufuasi wetu, na kwa maana hiyo, tudumu katika Kristo aliye Mchungaji mwema tukimtolea kwa uaminifu, sasa na hata milele.
Amina.
Uwe na Jumatano njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650