Date: 
30-04-2025
Reading: 
Warumi 1:1-7

Hii ni Pasaka

Jumatano asubuhi tarehe 30.04.2025

Warumi 1:1-7

[1]Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu;

[2]ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu;

[3]yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili,

[4]na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu;

[5]ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake;

[6]ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo;

[7]kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.

Yesu ajifunua kwetu;

Mtume Paulo anaanza kuandika Waraka kwa Warumi kwa salamu, akijitambulisha kama aliyetumwa kuhubiri Injili, lakini zaidi akimtangaza Yesu Kristo kama Mwokozi aliyekuja duniani akateswa na kufa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu. Mtume Paulo anasisitiza kuwa ni katika Kristo, wote waaminio wamekuwa wateule. Mtume Paulo anaonekana kuitika wito wa kuhubiri habari njema. Ndio maana Salamu yake ina ujumbe wa Yesu Kristo.

Mtume Paulo anaitika kuhubiri Injili. Kwa kuitika wito huo maana yake Yesu alijifunua kwake naye akaitika. Sisi tumeitika? Yesu anapojifunua kwetu anatuita kumfuata katika hali zote. Maisha tunayoishi yawe ya kumcha yeye. Tumtegemee yeye katika kazi zetu, maana yeye ndiye kiongozi wetu. Yesu anajifunua kwetu ili tumfuate. Mwamini sasa uokolewe. Amina

Jumatano njema

 

Heri Buberwa