
Tarehe 18 Aprili 2025 ilifanyika ibada takatifu ya kuadhimisha Siku ya Ijumaa Kuu katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front, ibada ambayo iliwakutanisha washarika na wageni mbalimbali ili kukumbuka siku ambayo Yesu Kristo aliteswa na kufa msalabani kabla ya kufufuka siku ya tatu.
Somo: Yesu Alikufa Msalabani Kwa Ajili Yetu ~ Luka 23: 44 - 49
Akizungumza katika moja ya ibada za siku hiyo Msaidizi wa Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dean Chediel Lwiza alisema kuwa mateso ya Yesu Krsito pale msalabani yanatukumbusha juu ya ukuu wa Yesu na namna ambavyo hata watu ambao hawakuwa na imani juu ya uweza wake kuwa waliamini siku hiyo kutokana na matendo makubwa yaliyotokea. Dean Lwiza alimzungumzia Akida, ambaye katika maandishi matakatifu anatajwa kuwa askari aliyekabidhiwa jukumu la kuhakikisha anasimamia mateso na kufa kwa Bwana Yesu. Dean Lwiza anasema licha ya Akida kuwa askari na mtu aliyetekeleza mauaji mengi hapo awali, hakusita kukiri mbele ya viongozi wake (akiwemo Pilato, Kayafa, Makuani na Askari wenzake) juu ya Ukuu wa Yesu Kristo kutokana na mambo aliyoyashuhudia wakati akitekeleza hukumu ya Yesu msalabani.
"Mungu anaweza kufanya mambo ambayo akili zetu na mawazo yetu hayawezi kupokea haraka. Pia wakati mwingine yanaweza kutokea mambo makubwa hata mimi, hata wewe ukastaajabu. Huyu muuaji (Akida) anatuambia hayo mambo makubwa matatu aliyoyatenda (1. Kumtukuza Mungu, 2. Kumsifu Mungu & 3. Kumheshimu Mungu) ni kwa sababu moja tu, Yesu alikuwa ni mwenye haki. Lakini vilevile akamwita kuwa alikuwa ni Mwana wa Mungu." alisema Dean Lwiza.
46 Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. 47 Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki.
"Sisi wakristo Mungu ametupa neema ya kumjua Yesu, neema ya kumjua Mungu na neema ya kumjua Roho Mtakatifu. Lakini inawezekana tukakaa naye muda mrefu sana tukashindwa kufanya kitu chochote ambacho Mungu angetegemea mimi na wewe tungefanya. Huyu ndugu (Akida), alimtukuza Mungu, Alimsifu Mungu, Alimheshimu Mungu na alienda kuwaambia wengine kuwa huyu (Yesu) ni mwana wa Mungu. Maana yake nini, kifo cha Bwana Yesu kimeleta watu waili na kuwaingiza kwenye uzima wa milele, wa kwanza jambazi pale msalabani, wa pili huyu muuaji (Akida) ambaye alikiri hadharani kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.
Ni jambo gani leo ukiona kifo cha Yesu tunachokizungumza, likekujenga au kukubadilisha? Mungu atusaidie na Yesu Kristo neema yake atusaidie tunapokiona kifo chake na kufa kwake, ana madai na sisi. Hawezi kufa tu msalabani hivi hivi, akaondolewa utu wake hivi hivi. Ana madai na wewe." alisema Dean Lwiza.
Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front, Chaplain Charles Mzinga aliwapongeza washarika wote walioshiriki katika kuandaa na kuigiza katika igizo la Pasaka la mwaka 2025.
Baadhi ya matukio katika picha kutoka kwenye Ibada za Siku ya Ijumaa Kuu (tazama hapa chini).
Tazama ibada za Siku ya Ijumaa Kuu hapa.
1. Ibada ya Kiswahili (Swahili service): https://www.youtube.com/watch?v=878FGuKiKnA
2. Ibada ya Kiingereza (English Service): https://www.youtube.com/watch?v=5Y8k_3OYG5Y
3. Ibada ya Kiswahili (Swahili service): https://www.youtube.com/watch?v=s8YxeFxCqVs
-------------######----------------