Hii ni Pasaka;
Jumatano asubuhi tarehe 23.04.2025
Yohana 21:15-17
[15]Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda
kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda.
Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.
[16]Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu.
[17]Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.
Tembea na Yesu mfufuka.
Usiku wa Jumapili ya Pasaka na siku iliyofuata, Yesu aliwatokea wanafunzi wakiwa wamejifungia chumbani kwa hofu ya wayahudi. Baada ya kuwatokea tena wakiwa na Thomaso Juma moja baadaye, inaonekana waliendelea na maisha yao ya zamani kama kawaida.
Kutokewa kwao na Yesu kulidhihirisha ufufuko, lakini bado walienda kuendelea na kazi zao walizozifanya zamani. Walienda kuvua samaki. Hawakuvua kwa kupumzika au kufurahi, bali walivua samaki ili waishi. Wao baada ya kutokuwa na Yesu ana kwa ana, walirudi kwenye kazi yao ya awali.
Tukirudi katika maisha yetu;
Baada ya kuijua Injili ya kweli iletayo wokovu, na baada ya kuona ukweli usio na shaka kuwa Yesu kweli alifufuka, nini itikio letu katika kuuendeleza utume wa Kristo Yesu?
Injili ya leo inatuonesha jinsi Petro alivyoitikia ufufuko wa Yesu. Tunaweza kusema alikuwa mvuvi kiongozi. Alikuwa amerudi kwenye kazi aliyoijua, aliyoimudu, na aliyoifanya kwa furaha kabisa. Lakini pamoja na kuwa mvuvi mjuzi, alivua usiku bila kupata chochote
Yohana 21:3
[3]Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu.Ni Yesu alipowajia akawaambia kutupa jarife, tena wakati kunapambazuka ndipo wakapata samaki wengi, kiasi cha kushindwa kulivuta jarife.
Hapa ni dhahiri inawezekana wavuvi wenzake na Petro waliona si mjuzi tena kwenye hiyo tasnia, yeye kama kiongozi wao.
Lakini hadi hapo kwanza, tumaweza kujifunza kuwa sio kila kitu tunachofanya tutegemee majibu tuliyoyazoea. Ni muhimu kutafiti na kujifunza zaidi, maana zipo changamoto katika mazingira ya kazi kila wakati. Muhimu ni kuwa juhudi yenye maarifa, tukimtanguliza Yesu.
Tuendelee;
Baada ya kurejea pwani, Yesu aliwapatia kifungua kinywa. Aliwapa mkate na samaki waliovua. Wakashiba. Walikuwa wamechoka usiku kucha tena bila kupata kitu, hivyo bila shaka walikuwa na njaa. Kutofanikiwa usiku kuliwakatisha tamaa. Lakini sasa mwenye nguvu ya kutuliza bahari aliweza kuwafuta machozi, na kuwainua tena.
Kumbuka, mara ya mwisho walikula na Yesu Alhamis, ambapo aliwaosha miguu. Sasa asubuhi hii wakaanza kukumbuka mambo yaliyopita, yaani kulishwa na Yesu na kuoshwa miguu.
Ndipo katika somo la leo Yesu anaongea na Petro akimwambia kuhusu kulisha kondoo zake. Anamuuliza mara tatu, na Petro anahuzunika (17).
Petro anahuzunika baada ya kuulizwa mara tatu na Yesu kama anampenda. Kumbuka Ijumaa Kuu tuliona Petro akimkana Yesu mara tatu kabla ya Jogoo kuwika. Katika hali ya kawaida lazima alishuka! Mara tatu tena? Labda aliona Bwana ana mashaka naye?
Petro alikuwa ameona Yesu amekufa, na alihakiki ufufuko wa Yesu kaburini, lakini akawa amerudi kuvua samaki! Yesu alikuwa anamtuma kwa msisitizo.
Turudi nyuma kidogo;
Yesu anamuita Simoni wa Yohana na siyo Petro, kwa nini? Muhimu kufahamu ilikuwaje akapewa jina Petro;
Mathayo 16:13-18
[13]Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? [14]Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. [15]Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? [16]Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. [17]Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. [18]Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.Yesu alimuita Petro baada ya kuona Imani yake kubwa sana. Kwa Imani ile alimuona mwamba. Lakini baadaye Petro akamkana Yesu mara tatu! Lakini Yesu aliendelea kumuita Petro, labda tu katika somo la leo, ambapo alimuona kuyumba kiimani. Ndio maana anamuuliza, "Je wanipenda?"
Hapa kuna umuhimu tuone neno upendo lilivyotumika na Yesu;
Kwa Kiyunani, neno Upendo liko hivi;
1. Eros-Upendo wa kawaida (physical love)
2. Phileo-Upendo wa ndugu (brotherly love)
3. Agape-Upendo wa kiMungu (Divine love)
Wakati Yesu akimaanisha Upendo wa kiMungu (Agape) Simon Petro anajibu kuwa anampenda Yesu kama ndugu yake (brotherly) hali iliyosababisha Yesu kurudia mara tatu. Kama tulivyoona hapo awali, anayeulizwa anaumia sana baada ya kuulizwa mara tatu, akikumbuka kumkana Yesu mara tatu na jogoo kuwika siku chache zilizopita.
Yesu bado aliitaka Imani ya Petro.
Kuuliza swali mara nyingi swali lile lile kwa mwanafunzi yule yule ni njia mojawapo ya kukaza somo husika. Yesu anapouliza mara ya tatu ni mkazo kwa Petro kueleza anachomuitia.
Pamoja na Imani, kwa lugha ya leo unaweza kusema alikuwa na "majanga". Unakumbuka alitembea juu ya maji, lakini mara ghafla akaanza kuzama? Baadae ndiye anamkana Yesu! Lakini bado Yesu alimwamini Petro, akimuona kiongozi wa Kanisa lake hata akiisha kupaa.
Kama alivyomuita Petro, Yesu nasi anatuita na kututuma kulilisha kundi lake, yaani kuhubiri Injili kwa wote. Nini nafasi yako katika hili?
Tunampenda Yesu?
Maisha yetu yanaakisi kumpenda Yesu?
Kutembea na Yesu mfufuka ni kumpokea mioyoni mwetu, na kumfanya kiongozi wa maisha yetu.
Yesu aliyetuita anatuagiza kumpenda na kulisha kondoo wake. Kulisha kondoo wake ni kuifanya kazi yake bila kuchoka.
-Kumpenda Yesu kunatokana na uhusiano wetu naye.
-Kumpenda Yesu ni matokeo ya kutambua neema yake.
-Kumpenda Yesu kunatutaka kuwa watu wa toba pale tunapokosa.
-Kama unampenda Yesu, lisha Kondoo zake.
Nakuacha na swali;
"Unampenda Yesu"?
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650