Date: 
20-04-2025
Reading: 
Marko 16:1-8

Hii ni Pasaka;

Jumapili ya tarehe 20.04.2025

Siku ya kukumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo;

 

Masomo;

Zab 118:7-14

1Kor 15:35-49

*Mk 16:1-8

 

Marko 16:1-8

1 Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka.

2 Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza;

3 wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi?

4 Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno.

5 Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu.

6 Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka.

7 Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.

8 Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingia tetemeko na ushangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa. 

Yesu mfufuka ni tumaini la wote waaminio;

Marko anaandika kwa ufupi akionesha wanawake watatu kwenda kununua manukato baada ya sabato, na alfajili iliyofuata walikwenda kaburini wakitaka kumpaka Yesu. Walikuwa wakiwaza ni nani angewaondolea jiwe kaburini ili watimize azma yao. Marko anawataja kwa majina wanawake walioshuhudia kusulubiwa, kuzikwa na kufufuka kwa Yesu (Mk 15:40,47; 16:1)

Ilikuwa ni desturi ya wayahudi kupaka miili mafuta ili kuondoa harufu mbaya, lakini kuonesha upendo. Wanawake waliotajwa kwenye somo la leo hawakutegemea kumkuta Yesu hai, japokuwa alikwisha kusema kuwa angefufuka siku ya tatu (Mk 8:31, 9:31, 10:34)

Yohana anaandika kuwa Mariam Magdalene alikwenda kaburini mapema;

Yohana 20:1

Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini.

Wanawake wengine wawili waliungana naye baadaye. Lakini Marko anaandika juu ya wanawake watatu wakijadiliana nani angewaondolea jiwe kaburini (Mk 16:3). 

Somo letu liaonesha kaburi likiwa wazi (4-6). Wale wanawake walipofika walikuta kaburi likiwa wazi, jiwe likiwa limeondolewa, japokuwa lilikuwa kubwa sana. Ndipo wakapewa ujumbe wasishangae, maana waliyemtafuta amefufuka. 

Nani aliliondoa jiwe?

Marko haelezi nani aliliondoa jiwe kaburini. Anaeleza tu, kuwa wanawake walipofika walikuta jiwe limeondolewa (4). Jiwe halikuondolewa ili Yesu atoke, maana angeweza kutoka hata kwa uwepo wa jiwe. Jiwe lilitolewa kutangaza kuwa "kaburi li wazi". Jiwe kuwa pembeni mwa kaburi lilikuwa tangazo la kufufuka kwa Yesu.

"Injili ya Mathayo hueleza kuwa malaika aliliviringisha jiwe akalikalia. Halikuwekwa pembeni ili lirudishwe baadae, bali lilisukumwa pembeni kwa nguvu ya pekee, likikaa kama sehemu ya kukaa kwa ajili ya malaika aliyesubiri hadi wanawake kufika kaburini..." (Lenski RCH)

Malaika alikuwa pale kulinda ushahidi wa kaburi. Yeye ndiye aliyetoa ujumbe wa kufufuka. Hapa ndipo kuna historia ya ukombozi katika ukristo. 

Inaandikwa kwa ufupi, lakini katika hali ya kawaida lazima wanawake waliogopa na kushtuka! Lakini malaika anaondoa hofu hiyo anapotangaza ufufuko.

Zilifanyika juhudi kuficha ukweli wa kufufuka kwa Yesu kwa kusema uongo;

Mathayo 28:11-15

11 Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka.
12 Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi,
13 wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala.
14 Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi.
15 Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.

Hadi leo wapo wasioamini wala kukubali kuwa Yesu alifufuka! Japokuwa Injili tuliyosoma inabainisha hilo, kuwa Yesu alifufuka. 

Kuamini tu kuwa Yesu alifufuka haitoshi, bali kumpokea na kumpa maisha yetu. Yaani tufufuke naye. Tunapoamini katika ufufuo tuzingatie yafuatayo;

1.Mungu aliliondoa jiwe kuweka ushahidi wa kaburi wazi, kuwa Yesu alifufuka. 

Alitumia malaika (Math 28:2). Kulikuwa na tetemeko la nchi pia. Kuondolewa kwa jiwe lilikuwa tukio la kiMungu kuwahakikishia wanawake na wanafunzi kuwa Yesu alifufuka. Amini katika tangazo, kuwa Yesu alifufuka kwa ajili yetu.

2.Yesu alikuja kwa sababu ya dhambi zetu, na alifufuka tena tuhesabiwe haki;

Warumi 4:25

ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.

3.Kufufuka kwa Yesu ni uthibitisho kuwa yeye ni mwana wa Mungu;

Warumi 1:4

Na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu;

Hii inadhihirisha kuwa Yesu ni Mungu kweli, na kwa kufufuka kwake tumepatanishwa na Mungu. Wewe umepatanishwa naye?

4.Kufufuka kwa Yesu ni hakikisho kuwa kifo kilishindwa na "kufa na kufufuka" kwa Yesu.

Yesu anaishi, anatuita kuishi naye milele. Hii inaonesha gharama aliyolipa kwa ajili ya ulimwengu. Yaani hatudaiwi chochote. Tunaitwa kumwendea Yesu mfufuka, ili mwisho wetu uwe mwema.

5."Maelfu huoshwa kwa maji ya Sakramenti, ambao hawajaoshwa kwa damu ya Kristo.... Maji ya ubatizo peke yake hayaleti neema.." (J C Ryle)

Nukuu hii inatufundisha umuhimu wa imani ya kweli katika Kristo kwa ajili ya wokovu. Siyo kwa ubatizo tu, kuwa msharika maarufu, kazi njema, Sakramenti n.k bali yote hayo yawe katika imani ya kweli katika Kristo mfufuka. 

1 Petro 1:3

Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;

 

6.Nini itikio letu kwa Yesu aliyefufuka?

Warumi 10:9-10

9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.

Nini itikio lako wewe kwa Yesu aliyefufuka?

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com