Date: 
18-04-2025
Reading: 
Luka 23:44-49

Hii ni Ijumaa Kuu;

Siku ya kukumbuka kifo cha Bwana Yesu;

Terehe 18.04.2025

 

Masomo;

Zab 22:1-4

Zek 13:7-9

*Lk 23:44-49

 

Luka 23:44-49

44 Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda,

45 jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.

46 Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.

47 Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki.

48 Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua.

49 Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.

Yesu alikufa msalabani kwa ajili yetu;

Luka anaandika kwamba Yesu alikuwa msalabani kwa karibu saa tatu, mchana kukawa na giza nene juu ya nchi. Mwanga wa jua ulishindwa, ulikoma. Luka anatumia neno la Kiyunani "ekleipo" akimaanisha "kushindwa", "kuharibika". Jua halikupatwa, jua halikutiwa giza, wala kuzuiwa, bali mwanga kutoka kwenye jua uliondoka, ndicho Luka anachoandika. Luka anatumia neno "ekleipo" katika maeneo mengine mawili akimaanisha "kushindwa/kuharibika/kukosa". Angalia;

Luka 16:9

Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili "itakapokosekana" wawakaribishe katika makao ya milele.

Luka 22:31-32

31 Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano;
32 lakini nimekuombea wewe ili imani yako "isitindike"; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.

Hatujui giza lilikuwa kwa umbali upi. Neno lililotafsiriwa "nchi" laweza kumaanisha "dunia". Hivyo hatujui kama giza lilikuwa Yerusalemu tu, au katika Israeli yote, Mediterranean, au dunia nzima. Tunachoweza kujua ni kuwa Mungu alikuwa nyuma ya tendo hili. Giza huwakilisha hukumu ya Mungu katika unabii wa Agano la kale (Zefania 1:14-25, Amosi 5:20, Amosi 8:8-10)

Tuangalie mfano wa Nabii Amosi alivyotabiri;

Amosi 8:9-10

9 Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru ya mchana.
10 Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu.

Amosi hakuwa anatabiri kuhusu siku ya kusulibiwa kwa Yesu. Giza liliwakilisha hukumu ya Mungu kwa wasioamini. Giza kuwepo iliashiria hukumu kwa watu ambao hawakumwami Yesu. Mara kadhaa baadhi yetu wamesema giza ilikuwa umoja kati ya Baba na Mwana. Katika Injili hakuna mahali kinaonekana kitu kama hicho. 

Niweke sawa hapa; giza halikumaanisha hukumu ya Mungu kwa Yesu, bali hukumu kwa Israeli wote ambao hawakumpokea. Kusulibiwa kwa Yesu ilikuwa kuelekea ukombozi wa wanadamu, na giza lilikuwa ishara ya hukumu kwa wasioamini.

Tukio lingine la kustaajabisha ni pazia la hekalu kupasuka (45). Pazia lilipasuka, na tukumbuke kwamba ilikuwa maandalizi ya Pasaka. Sehemu ya patakatifu pa patakatifu ilikuwa sehemu ndogo iliyotengwa mahali ambapo upatanisho ulifanyika mara moja kwa kila mwaka. Hakuna aliyeruhusiwa kuingia sehemu ile takatifu, ni Kuhani Mkuu aliyeingia akiwa na damu za wanyama akifanya upatanisho kwa watu na Mungu. Kwa pazia la hekalu kupasuka, Yesu anafuta taratibu za Kuhani na damu za wanyama, akiwa yeye Kuhani Mkuu, aliye Mpatanishi na Mungu wetu kama mwandishi wa waraka kwa Waebrania anavyosema;

Waebrania 9:11-14

11 Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu,
12 wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele.
13 Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili;
14 basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?

Luka tena anaandika neno la mwisho la Yesu (hili huwa ni neno la Yesu la saba msalabani) pale aliposema "mikononi mwako naiweka Roho yangu". Na baada ya kusema maneno haya akakata roho. Haya maneno hayakutoka hewani, bali ni nukuu;

Zaburi 31:5

Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.

-Zaburi ya 31 ni sala ya mwenye haki anayeteswa katika mikono ya adui akiomba kukombolewa. Aliyesema maneno haya alikuwa anajiweka mikononi mwa Mungu. Ndicho Yesu alichofanya, anaungana tena na Baba yake. Yesu hakutolewa msalabani, hakukuwa na ishara wala Mungu kuzuia kama alivyoomba kikombe kimuepuke, lakini bado alikufa akiwa katika uhusiano mzuri na Baba yake.

Yesu alikufa msalabani kwa ajili yetu;

Matukio tuliyoyasoma kwenye somo la Ijumaa kuu leo (giza nene, pazia kupasuka, na kutamka neno la saba) yanadhihirisha Utukufu wa Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu aiondoaye dhambi ya ulimwengu. Mwandishi wa Waebrania anaandika;

Waebrania 6:19-20

19 tuliyo nayo kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia,
20 alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.

Kumbe kwa giza nene, tunakumbushwa kumwamini Yesu Kristo ambaye huweza kufanya hata yasiyowezekana. Kupasuka kwa pazia ni uhakika wa sisi kumwendea Yesu wenyewe wakati wowote, hatuhitaji mbuzi wala damu. Na kwa neno la saba, Yesu anaungana na Baba yake, akitukumbusha kujiweka mkononi mwa Mungu siku zote. Tunapoadhimisha Ijumaa Kuu, tukumbuke kuwa Yesu alikufa kwa ajili yetu, hivyo tutafakari juu ya njia zetu, ili kwa njia ya kifo chake tuurithi uzima wa milele. Amina

Tunakutakia ibada njema ya Ijumaa kuu

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com