Date: 
12-04-2025
Reading: 
Waebrania 10:1-7

Hii ni Kwaresma 

Jumamosi asubuhi tarehe 12.04.2025

Waebrania 10:1-7

1 Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.

2 Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi?

3 Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka.

4 Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.

5 Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari;

6 Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo;

7 Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.

Yesu ni Mpatanishi;

Mwandishi anaandika juu ya kafara kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa enzi za Agano la kale. Anaonesha kwamba zamani damu ya mafahali na mbuzi ilitumika kuondoa dhambi, yaani kuhani aliongoza watu kutoa sadaka ya kuteketezwa na alikwenda mbele za Mungu kwa sadaka hiyo ili watu wasamehewe. Kuhani alisimama kama Mpatanishi kati ya watu na Mungu, kwa sadaka za kuteketezwa.

Mwandishi sasa anasema damu ya mafahali na mbuzi haiwezi kuondoa dhambi. Kwa maneno ya mwandishi, kafara ya Kristo inatosha. Yesu alifanyika sadaka ili sisi tupatanishwe na Mungu. Hakuna sadaka nyingine yoyote ambayo tunaweza kutoa ili tuokolewe. Wokovu wetu na msamaha vinapatikana kwa njia ya Yesu Kristo pekee. Tumtazame yeye daima. Amina

Jumamosi njema

Heri Buberwa