Date:
05-04-2025
Reading:
Zaburi 104:10-15
Hii ni Kwaresma
Jumamosi asubuhi tarehe 05.04.2025
Zaburi 104:10-15
10 Hupeleka chemchemi katika mabonde; Zapita kati ya milima;
11 Zamnywesha kila mnyama wa kondeni; Punda mwitu huzima kiu yao.
12 Kandokando hukaa ndege wa angani; Kati ya matawi hutoa sauti zao.
13 Huinywesha milima toka orofa zake; Nchi imeshiba mazao ya kazi zako.
14 Huyameesha majani kwa makundi, Na maboga kwa matumizi ya mwanadamu; Ili atoe chakula katika nchi,
15 Na divai imfurahishe mtu moyo wake. Aung'aze uso wake kwa mafuta, Na mkate umburudishe mtu moyo wake.
Tutunze uumbaji (mazingira)
Zaburi ya 104 inamhusu Mungu muumbaji, atoaye. Mwimbaji wa Zaburi anaanza kwa kumsifu Mungu muumbaji wa ulimwengu na vyote vilivyomo pale anaposema;
Zaburi 104:1-4
1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Wewe, Bwana, Mungu wangu, Umejifanya mkuu sana; Umejivika heshima na adhama. 2 Umejivika nuru kama vazi; Umezitandika mbingu kama pazia; 3 Na kuziweka nguzo za orofa zake majini. Huyafanya mawingu kuwa gari lake, Na kwenda juu ya mabawa ya upepo, 4 Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali.Somo tulilolisoma ni mwendelezo wa sifa kwa Mungu muumbaji. Tunaona Mungu alivyoumba milima na mabonde, wanyama na ndege wa angani. Ndiye aliyeumba mimea yote, kwenye ardhi iletayo mazao ya kutosha. Kama mwimbaji anavyomsifu Mungu, nasi tumsifu na kumshukuru kwa kutunza uumbaji wake, ili dunia iwe sehemu salama kwa viumbe vyote. Amina
Jumamosi njema
Heri Buberwa