Hii ni Kwaresma
Jumamosi asubuhi tarehe 29.03.2025
Luka 9:51-56
51 Ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu;
52 akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.
53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu.
54 Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?
55 Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]
56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine.
Tumtazame Bwana aliye tumaini;
Yesu kabla ya kuingia katika kijiji cha Wasamaria alituma ujumbe kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji wa Samaria hawakumkaribisha kama yeye alivyokuwa amewaendea. Wanafunzi wa Yakobo na Yohana wakapendekeza waagize moto ushuke toka mbinguni uwaangamize watu wa Samaria! Yesu akawajibu kuwa hakuja kuangamiza bali kuokoa.
Wanafunzi wa Yakobo na Yohana bado walitawaliwa na tamaduni za Agano la kale, adhabu juu ya adhabu. Yesu yeye anaonesha neema kwa kutaka kuokoa watu ambao hawakumkaribisha. Neema ya Kristo hudumu hata sasa, akiwaokoa wote wamwaminio na kumfuata. Tuendelee kumtazama yeye tu, ili tuwe na mwisho mwema. Amina
Jumamosi njema
Heri Buberwa