Date: 
28-03-2025
Reading: 
Yohana 11:1-11

Hii ni Kwaresma 

Ijumaa asubuhi tarehe 28.03.2025

Yohana 11:1-11

[1]Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake.

[2]Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi.

[3]Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi.

[4]Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo.

[5]Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro.

[6]Basi aliposikia ya kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo.

[7]Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena.

[8]Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena?

[9]Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu.

[10]Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake.

[11]Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha.

Tumtazame Bwana aliye tumaini;

Lazaro wa Bethania alikuwa amefariki na alikuwa tayari amezikwa kaburini kwa siku nne (17). Ujumbe ulitumwa kwa Yesu kuhusu kifo cha Lazaro, naye akawaamuru wanafunzi kuelekea Uyahudi tena akiwa nao, mahali ambako siku chache zilizopita walitaka kumpiga kwa mawe! Wakati akielekea kumponya Lazaro, Yesu anasema Lazaro amelala tu, ninakwenda nipate kumwamsha! Hii ilikuwa mshangao kwa mtu ambaye ilijulikana amekufa, amezikwa!

Hata baada ya kufika eneo la tukio, ufufuo wa Lazaro kama ambavyo ilikuja kutokea haukutegemewa. Mfano ni maongezi ya Martha na Yesu;

Yohana 11:23-27

23 Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka.
24 Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.
25 Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;

26 naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?

27 Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.

Bila shaka watu walikusanyika, na hatimaye Yesu akaamuru jiwe liondolewe kaburini, Lazaro akafufuka na huzuni ya ndugu zake Lazaro ikaondoka. Ishara hii hutumika na baadhi ya mitume na manabii wa leo "kufufua watu kama Yesu". Sisi tuzingatie kuwa na uhusiano mwema na Yesu ili tufe katika yeye. Lazaro aliyefufuliwa hakuishi milele, alikufa. Hata wengine wote waliofufuliwa na Yesu hawapo sasa, walikufa. Kufufuliwa kwa Lazaro na Yesu kutukumbushe kuwa Yesu ndiye tumaini letu, lakini tusiiache imani ili tufe katika yeye. Amina

Ijumaa njema

Heri Buberwa