Hii ni Kwaresma
Alhamisi asubuhi tarehe 27.03.2025
Kutoka 13:17-22
17 Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri;
18 lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha.
19 Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.
20 Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa.
21 Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku;
22 ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.
Tumtazame Bwana aliye tumaini;
Farao alikuwa na moyo mgumu sana kuwaachia wana wa Israeli kuondoka Misri, ila baada ya mapigo kumi aliwaruhusu waondoke. Hakuridhika, bado aliendelea kuwafuatilia, ndiyo maana jeshi lake (Farao) liliangamia kwa kuzama baharini. Baada ya kuruhusiwa kuondoka, wana wa Israeli walipewa taratibu za jinsi ya kumtolea sadaka mzaliwa wa kwanza, na jinsi ya kusherehekea Pasaka. Safari ikaanza.
Ndipo tunaona katika somo leo Mungu akiwaongoza Israeli kwa njia aliyoitaka yeye. Aliwatangulia usiku na mchana, wingu likiwaongoza mchana na kuwa nguzo ya moto usiku. Ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku mbele ya wana wa Israeli. Mungu alikuwa kiongozi wao. Nasi tukimtazama Bwana anatuongoza daima. Amina
Siku njema
Heri Buberwa