Date:
25-03-2025
Reading:
Mwanzo 39:21-23
Hii ni Kwaresma
Jumanne asubuhi tarehe 25.03.2025
Mwanzo 39:21-23
21 Lakini Bwana akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.
22 Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya.
23 Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu; kwa kuwa Bwana alikuwa pamoja naye. Bwana akayafanikisha yote aliyoyafanya.
Tumtazame Bwana aliye tumaini;
Yusufu baada ya kuwa ameuzwa Misri na ndugu zake, sasa ni mtendakazi katika nyumba ya Potifa. Humo ndani pamoja na kupewa mamlaka na Potifa, mke wa Potifa alimuingiza majaribuni kwa kutaka alale naye. Yaani mke wa Potifa alitaka kuzini na Yusufu. Yusufu kwa sababu ya kumcha Bwana alikimbia, nguo yake ikabaki mikononi mwa mke wa Potifa! Mke wa Potifa ndipo akautangazia umma kwamba Yusufu alitaka kumbaka! Mfalme akamtia Yusufu gerezani.
Somo la asubuhi hii linaanzia hapo, kwamba baada ya Yusufu kutiwa gerezani, Mungu alikuwa naye, hata akapata kibali mbele ya mkuu wa gereza. Wafungwa wote wakawa chini ya Yusufu! Bwana alimfanikisha Yusufu huko gerezani. Yusufu alisingiziwa akawekwa gerezani, lakini akakutana na mkuu wa gereza aliye mwema. Yusufu alimtazama Bwana katika yote, wito ambao tunapewa asubuhi kwamba tumtazame Bwana aliye tumaini letu ili tuwe na mwisho mwema. Amina.
Jumanne njema
Heri Buberwa