Hii ni Kwaresma
Ijumaa asubuhi tarehe 21.03.2025
Kutoka 1:8-14
8 Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu.
9 Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi.
10 Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii.
11 Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi.
12 Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli.
13 Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali;
14 wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali.
Tupinge ukatili kwa Neno la Mungu;
Yusufu mwana mpendwa wa Yakobo aliuzwa na ndugu zake kwa Waishmael akapelekwa Misri, kwa sababu Yakobo alimpenda sana Yusufu, jambo ambalo ndugu zake halikuwapendeza. Huko Misri alipitia tabu nyingi ikiwemo kufungwa gerezani, kusingiziwa n.k lakini mwishowe akaja kuwa kiongozi mkubwa ndani ya Misri baada ya Farao. Shida ya njaa ilisababisha wana wa Yakobo nao wakahamia Misri, sababu ya kiongozi Yusufu.
Sasa Yusufu akafa kama tunavyosoma;
Kutoka 1:6-7
6 Yusufu akafa, na ndugu zake wote, na watu wote wa kizazi kile. 7 Na wana wa Israeli walikuwa na uzazi sana, na kuongezeka mno, na kuzidi kuwa wengi, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao.Somo letu linaanzia hapo, kwamba alikuja mtawala mpya kuitawala Misri ambaye hakumjua Yusufu. Somo linaonesha Waisraeli wakiishi maisha magumu ya mateso kwa sababu ya mtetezi wao kutokuwepo tena! Walikuwa wengi, wenye uzao, wakawa tishio kwa Wamisri! Lakini Wamisri walivyozidi kuwatesa ndivyo walivyozidi kustawi. Waisraeli wakaendelea kutumikishwa kwa ukatili. Baada ya muda mrefu Bwana aliwaokoa kutoka utumwani Misri na kuwarudisha kwenye nchi yao ya ahadi.
Wamisri waliwatumikisha Waisraeli kwa sababu waliwaona tishio. Huu ulikuwa ukatili, na haujaaza leo. Hata leo iko tabia ya baadhi yetu kutumia mamlaka yetu kuumiza wengine kwa maslahi yetu binafsi, yaani tuko tayari kufurahi wakati wenzetu wakiumia! Hii haikubaliki! Tumia nafasi yako kwa Utukufu wa Mungu, na siyo kwa utukufu wako! Ukatili ni dhambi. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa