Date: 
20-03-2025
Reading: 
Zaburi 10:1-12

Hii ni Kwaresma 

Alhamisi asubuhi tarehe 20.03.2025

Zaburi 10:1-12

1 Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida?

2 Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.

3 Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.

4 Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Hatapatiliza. Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu;

5 Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awafyonya.

6 Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni.

7 Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,

8 Hukaa katika maoteo ya vijiji. Mahali pa siri humwua asiye na hatia, Macho yake humvizia mtu duni.

9 Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Akimkokota wavuni mwake.

10 Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake.

11 Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe.

12 Bwana, uondoke, Ee Mungu, uuinue mkono wako, Usiwasahau wanyonge.

Tupinge ukatili kwa neno la Mungu;

Zaburi ya kumi ni Zaburi ya maombolezo inayoakisi shida kati ya mwovu na haki, kuonesha kwamba Mungu hayupo karibu na anayeteseka, ili kuingilia kati na kumuokoa mwenye haki huyo anayetaabika. Mwimbaji wa Zaburi analalamikia haki iliyopotea kwa sababu ya waovu, akimuuliza Mungu "kwa nini wasimama mbali?". Kwa tumaini, mwimbaji ambaye ni Daudi anamsihi Bwana kutowasahau wanyonge.

Daudi anaonesha waovu ambao ni wakorofi, wachoyo, watumiao nguvu na mamlaka kuumiza wengine kwa manufaa yao. Matendo yote haya na mengine yanayofanana nayo ni ukatili, hayafai! Majira haya yatukumbushe kumrudia Bwana kwa kutenda yatupasayo tukiacha na kupinga ukatili. Ukatili ni uovu! Amina

Alhamisi njema

Heri Buberwa