Date: 
13-03-2025
Reading: 
1Petro 3:3-18

Hii ni Kwaresma 

Alhamisi asubuhi tarehe 13.03.2025

1 Petro 3:13-18

13 Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?

14 Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu.

15 Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.

16 Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo.

17 Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.

18 Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,

Mungu hutuwezesha kushinda majaribu;

Petro anaandika juu ya mateso katikati ya kutenda haki, kwamba katika maisha ya ufuasi yako mateso, lakini waaminio sharti wakae katika njia ya haki. Ndiyo maana Petro anaelekeza kuwa ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ni mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. 

Msisitizo wa Petro ni kuishi kwa kutenda yawapasayo waaminio, hata katikati ya mateso. Kwa tafakari ya juma hili, naweza kusema kuwa ni muhimu kutenda yatupasayo katikati ya majaribu. Yaani majaribu yasitutoe katika njia sahihi ya imani yetu, bali tumtegemee Mungu ili kuyashinda hayo majaribu. Amina.

Alhamisi njema

Heri Buberwa