Hii ni Kwaresma
Jumatano asubuhi tarehe 12.03.2025
Yakobo 1:12-18
[12]Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.
[13]Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu.
[14]Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.
[15]Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.
[16]Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike.
[17]Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.
[18]Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Mungu hutuwezesha kushinda majaribu;
Yakobo anatusihi kustahimili majaribu ili tuweze kuipokea taji ya uzima. Lakini katika hilo, anatukumbusha kuwa tunajaribiwa kwa tamaa zetu wenyewe. Hivyo tuache tamaa ambazo zinaweza kusababisha tujaribiwe na hatimaye mauti.
Tunapoendelea na majira haya, tukumbuke kuwa majaribu yapo, na hatuwezi kuyakwepa. Ni kwa neno la Mungu tunaweza kuyashinda. Mstari wa 18 unasema alituzaa kwa neno la kweli. Huu ni msisitizo kuwa hatuwezi kushinda majaribu bila neno la Mungu.
Nakutakia siku njema
Heri Buberwa