
Siku ya Jumapili, Machi 9, 2025 ilifanyika ibada ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front. Ibada za aina hii hufanyika kila Jumapili ya kwanza ya mwezi Machi kila mwaka ili kutoa fursa kwa wanawake kuongoza matukio na huduma zote za ibada.
Akizungumza katika ibada hiyo, Mama Anna Mzinga (mhubiri wa siku), aliwapongeza wanawake na washarika wote kwa kufanikisha kufanyika kwa ibada hizo. Mama Mzinga alisoma neno la siku kutoka katika kitabu cha Luka 22: 40 – 46; Somo: Mungu Hutuwezesha Kushinda Majaribu.
Kupitia somo la siku hiyo, Mama Mzinga aliwaasa wanawake na washarika wote waliohudhuria ibada hiyo kumtegemea Mungu na kumwomba awawezeshe kushinda majaribu wanayokabiliana nayo katika shughuli zao za kila siku. “Kuna watu wengi karama zetu zimefia mahali kwasababu hatukuweza kusimama kwenye jaribu, tukakubali tamaa zetu zikatusukuma. Nafasi Mungu aliyokupa, mamlaka Mungu aliyokupa yakafia mahali kwasababu ulishindwa kukabiliana na jaribu. Neno la leo linatukumbusha kwamba ni Mungu peke yake ndiye anayeweza kutuwezesha kushinda majaribu,” alisema.
Katika ibada zote tatu zilizofanyika katika usharika wa Azania Front; mahubiri, matangazo, kuongoza litrugia na huduma nyingine zote za ibada za siku hiyo ziliongozwa na wanawake wa usharika.
Akizungumza katika ibada hiyo, Mchungaji Kiongozi wa Usharika; Chaplain Charles Mzinga aliwapongeza wanawake kwa kuwezesha ibada zote za siku hiyo kufanyika kwa mafanikio makubwa.
Siku ya Wanawake katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front ilitanguliwa na Maombi ya Dunia kwa wanawake yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, ambapo wanawake wa Usharika waliungana na wanzao kutoka madhehebu mbalimbali katika maombi hayo.
PICHA: Matukio mbalimbali katika picha wakati wa ibada za Siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front. Picha: AZF Media Team.
Tazama ibada hizo hapa:
1. Ibada ya Kwanza (Kiswahili): https://www.youtube.com/watch?v=nuPWaRUzmPI&t=5984s
2. Ibada ya Tatu (Kiswahili): https://www.youtube.com/watch?v=21B8Ny-__EI
------------------------------------------MWISHO-----------------------------------------------