Date:
10-03-2025
Reading:
Marko 1:12-13
Hii ni Kwaresma
Jumatatu asubuhi tarehe 10.03.2025
Marko 1:12-13
12 Mara Roho akamtoa aende nyikani.
13 Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.
Mungu hutuwezesha kushinda majaribu;
Injili ya Marko inatupa picha ya Yesu yukoje ili tumfuate. Katika Mk 1:9-11, tunauona ubatizo wa Yesu, akitamkwa kama mwana mpendwa, mwokozi na mfalme katika tukio la ubatizo. Kwa kutawazwa kwake kama mwana wa Mungu akianza huduma yake, Yesu hapokelewi kwa raha, badala yake anaongozwa na Roho Mtakatifu kwa kazi ngumu, kukutana na shetani jangwani.
Maudhui ya somo hili yanamhusisha shetani. Mbali na shetani, Injili ya Marko pia huonesha pia mapambano ya Yesu dhidi ya pepo, asili, viongozi wa kiyahudi, na wakati mwingine wanafunzi. Somo la leo ni picha ya Yesu akijenga ufalme wake ndani ya upinzani mkali (Zaburi 2). Hivyo kujaribiwa kwa Yesu siyo mfululizo wa matukio ya bahati mbaya. Mungu anamuongoza Yesu jangwani. Tukio hili huandikwa na Injili zote, Marko akiandika kwa ufupi. Binafsi sasa, hapa nami najaribiwa na ufupi wa uandishi wa Marko, kuiendea Injili ya Mathayo inayoandika juu ya majaribu matatu, yalikuwaje, na Yesu alipambana nayo vipi. Marko hakusisitiza hili, japo ni muhimu tuone Yesu alivyoshinda majaribu.
Siku arobaini jangwani;
Kitu tunachokiona kwanza ni Yesu kukaa jangwani kwa siku arobaini. Hii namba 40 siyo ya hivi hivi tu. Israeli walikuwa jangwani kwa miaka 40 baada ya kuvuka bahari nyekundu (Kumb 8:2), Musa alikuwa mlimani Sinai kwa siku 40 mchana na usiku (Kut 34:28), Eliya aliongozwa kwa siku 40 usiku na mchana kuelekea mlima Sinai (Horebu) (1Fal 19:8). Katika hali zote hizo jangwa lilikuwa sehemu ya kumhakiki mhusika, akipimwa kiwango cha ukomavu kiimani, na ahadi ya kukombolewa. Israeli walikuwa jangwani kama jaribio la Imani, wakiahidiwa ukombozi kama wangekuwa watii kwa Mungu. Sasa tunaona jangwa kama sehemu ya jaribio. Ndiyo maana yuko jangwani mwanzoni mwa huduma yake, na ukumbuke Mungu alisema huyu ndiye mwanangu mpendwa ninayependezwa naye. Nini kiliendelea?
Shetani;
Yesu hakujaribiwa kidogo. Yesu alijaribiwa na shetani. Maandiko yanamuonesha shetani kama nafsi halisi. Kwa utamaduni, shetani huusianishwa na mabaya. Huwa tunamfikiria shetani kama ujinga, ushirikina, uovu n.k lakini shetani anaonekana kuwa nafsi ya uovu. Shetani hutajwa kama mwovu, mwongo;
Ufunuo wa Yohana 12:9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
Shetani siyo wazo tu au hadithi. Ni nafsi ya uovu. Angalia maandiko haya;
1 Yohana 3:8
Atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.1 Petro 5:8
Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.Tunachokiona ni mgogoro wa falme mbili na watawala wawili. Yesu mfalme na mtawala wa mbingu na dunia, ambaye anapambana na shetani aliye mkuu wa anga na mtawala wa giza. Tunaiona picha ya ushindi wa kiroho na vita kati ya giza na nuru. Naweza kusema hii ni vita kati ya Mungu na mwanaye Yesu Kristo, na mwanadamu aliyekataa kujisalimisha kwa Mungu.
Yesu alilindwa na malaika;
Marko anaonesha Yesu kuhudumiwa na malaika, kama njia ya Yesu kushinda majaribu ya shetani. Andiko la Kiyunani husema kuwa "malaika walimhudumia Yesu kwa siku zote arobaini jangwani". Mungu hakuwa na Yesu mwanzoni tu, bali wakati wote wa kujaribiwa. Hivyo katika wakati wote wa kujaribiwa Yesu aliendelea kuwa "mwanae mpendwa anayependezwa naye".
Akihubiri katika ibada ya majivu tar 02.03.2022, Mchungaji Joseph Mlaki wa Kanisa Kuu la Azania Front alisema kuwa, kuna wakati mzazi anaweza kuwa anamwadhibu mtoto aliyemkosea, lakini mtoto ndiyo kwanza anamkumbatia mzazi wake, pamoja na kuwa anachapwa. Ni kwa sababu mtoto anatambua kuwa huyo ndiyo mzazi wake, hana pa kwenda. Na mzazi pia pamoja na kumchapa mtoto, anaendelea kumpenda zaidi. Ndivyo Mungu wetu alivyo. Hutupenda na kutujali wakati wote. Mfano wa Yesu kuhudumiwa siku zote jangwani unaakisi upendo wa Mungu kwetu usiokoma wakati wote tuwapo majaribuni.
Mungu hutuwezesha kushinda majaribu;
Yesu alijaribiwa kwa njia tatu, ambazo ni sawa na zile Israeli walijaribiwa jangwani, na zile Adamu na Eva walijaribiwa bustanini, kama nasi tujaribiwavyo leo. Shetani hana ubunifu wowote. Anayo majaribu katika njia tatu kwa mbinu moja. Majaribu haya ni tamaa ya mwili, tamaa ya macho na fahari ya maisha kama ilivyoandikwa;
1 Yohana 2:16
Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.Hata katika Agano la kale, (Mwz 3:6) Shetani alitumia njia hizo hizo kwa Eva. Aliona matunda ya mti bora kwa chakuka (tamaa ya mwili) matunda yalivutia (tamaa ya macho) na kujitambua (fahari ya maisha)
Hivyo hivyo, tukirejea Injili ya Mathayo na Luka, Yesu alijaribiwa kwa njia tatu. Shetani alimtaka kubadili jiwe kuwa mkate (tamaa ya mwili), alimwonyesha milki za ulimwengu (tamaa ya macho) akamwambia ajitupe chini (fahari ya maisha)
Hayo ndiyo majaribu matatu ya shetani ambayo hata sisi tunajaribiwa.
Hapo nilitaka kukuonesha kuwa majaribu yalikuwepo, yapo na yataendelea kuwepo. Kama Bwana Yesu mwenyewe alijaribiwa, sisi hatuwezi kukwepa kujaribiwa.
Ujumbe wangu kwako;
-Mungu anaweza kuruhusu upitie nyakati ngumu ili baadae uwe tayari kwa huduma fulani. Yesu mwenyewe alipitia majaribu kabla ya kuanza huduma yake. Hivyo unapopitia wakati mgumu usiondoke kwa Yesu. Tunaitwa kuishi katika hali zote tukimtegemea yeye, na hata pale tunaposhindwa yeye hutushindia.
- Yesu ni mshindi akimshinda shetani, ili tuokolewe dhambini. Bila Kristo hakuna kushinda dhambi. Kristo alishinda kifo ili sisi tushinde dhambi. Yeye anayo nguvu ya kushinda dhambi, na huu ndiyo mwanzo wa mwisho wa shetani. Yesu alishinda majaribu ya shetani, akituondoa kwenye jangwa la dhambi. Kumbe hatuwezi kushinda dhambi kwa nguvu zetu wenyewe, ndiyo maana tukimtegemea Mungu tutashinda majaribu.
Utume mwema.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650