Date:
05-03-2025
Reading:
Isaya 1:18-20
Hii ni Kwaresma;
Jumatano ya majivu; tarehe 05.03.2025
Masomo;
Zab 139:1-10
Luka 13:1-5
*Isaya 1:18-20
Isaya 1:18-20
18 Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.
19 Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;
20 bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.
Tutubu na kumrudia Mungu;
Utangulizi;
Maudhui ya sura ya kwanza ya kitabu cha Isaya yanaonekana kujirudia katika sura nyinginezo za Isaya, ikiwemo hatma ya Yerusalemu, ibada sahihi na umuhimu wa toba. Wasomi wa Agano la kale husema kwamba sura ya kwanza ya Kitabu cha Isaya iliandikwa vile kukitambulisha kitabu chote, mstari wa kwanza ukikaa kama kichwa cha habari. Sura ya kwanza ni mwanzo wa maongezi ya Mungu na watu wake. Ingawa kupo kutokukubaliana juu ya muundo wa sura, zipo sababu za kuangalia mstari wa 2 hadi 20 kama ushairi ambao unaanza na kuishia na maneno yanayofanana (Bwana amenena V kinywa cha Bwana kimenena haya).
Hali hii inatufanya tuone kuwa Bwana anaongea na watu wake kuhusu uovu wao. Bwana anasema ng'ombe amjua Bwana wake, punda ajua kibada chake, lakini Israeli hamjui Mungu wake! (3) Ukiendelea kusoma, unaona Mungu akizikataa ibada za Israeli na sadaka zao. Bwana anasema anayo mali kuliko sadaka zao. Anawataka kuacha kuleta sadaka za ubatili akisema anazichukia. Anaendelea kusema wasipofanya toba ataficha macho yake asiwaone wanapotoa sadaka zao (11-15). Bwana anaendelea kuwaelekeza watu kujiosha, kujitakasa na kuacha kutenda mabaya. Anawaita kumrudia yeye (16-19)
Somo lenyewe;
Baada ya kuona utangulizi hapo juu, ndipo somo linawaita watu kufanya toba. Bwana anawaita watu kusemezana naye ili anasafishe dhambi zao. Mungu anawaita watu wa Yerusalemu kuwa na uhusiano mzuri na yeye, uhusiano ambao utawafanya kula mema ya nchi, kinyume cha hapo ni kuangamia. Somo linaonesha kuna kukubali na kukataa. Kukubali ni kuuina ufalme wa Mungu bali kukataa ni kuangamia. Hitimisho la somo linaturejesha karne ya 8KK katika Yuda, ambapo Mungu alitoa mwaliko kwa watu wake kumfuata. Hapa tunalo la kutafakari, kwamba tunamwabudu Mungu katika kweli? Tunatenda haki na kuisimamia kweli katika jamii tuliyomo? Bwana anapowaambia Israeli kwamba watakula mema ya nchi anamaanisha atarudi. Je, tunaishi tukijua atarudi hivyo tujiandae? Basi karibu, Yesu anatuita kusemezana naye, kutubu.
Tutubu na kumrudia Mungu;
Ujumbe tuliosoma walipewa Israeli kabla ya kwenda uhamishoni Babeli. Pamoja na uovu wao, bado Bwana aliwaita kusemezana nao. Leo tunapoanza majira ya mateso, tunakumbushwa jinsi Yesu alivyopitia njia ya mateso kwa ajili ya wokovu wetu. Kwa njia hiyo tunakumbushwa kuwa tunawajibika kudumu katika imani ya kweli, toba na msamaha ili kumrudia Mungu wakati wote. Yesu anatuita kusemezana naye, yaani kutubu ili akae kwetu na kutupa uzima wa milele. Hivyo tutubu na kumrudia Mungu. Amina
Tunakutakia Kwaresma njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650