Date: 
04-03-2025
Reading: 
Waebrania 2:14-18

Jumanne asubuhi tarehe 04.03.2025

Waebrania 2:14-18

14 Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,

15 awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.

16 Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu.

17 Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake.

18 Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.

Yesu anayaendea mateso Yerusalemu;

Sehemu hii ya sura ya pili ya waraka kwa Waebrania inaeleza jinsi Yesu alivyoshuka toka mbinguni akaacha enzi na utukufu, akaja kama mwanadamu kwa ajili ya Taifa la Mungu. Somo linaonesha Yesu alivyokuja kuwaweka huru wale wote ambao walikuwa katika utumwa wa dhambi. Yeye ndiye aliyekuwa na nguvu ya kuvunja mauti.

Kazi ya kuokoa ulimwengu ilikamilika Yesu alipokufa na kufufuka. Kama ilivyokuwa wakati wanaandikiwa Waebrania, hata sasa wokovu huu ni kwa ajili ya wote. Tunapokumbuka Yesu alivyoiendea njia ya mateso, tukumbuke ilikuwa kwa ajili yetu, bure. Ni kwa njia hiyo tumeokolewa. Tudumu katika wokovu huu, leo na daima. Amina

Jumanne njema

 

Heri Buberwa 

Mlutheri