Date: 
26-02-2025
Reading: 
Matendo 18:24-28

Jumatano asubuhi tarehe 26.02.2025

Matendo ya Mitume 18:24-28

24 Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko.

25 Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu.

26 Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.

27 Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu.

28 Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.

Neno la Mungu ni silaha imara;

Apolo alikuwa Myahudi aliyekuwa hodari katika maandiko. Alipofika Efeso akaanza kuhubiri kwenye kusanyiko. Alifundisha habari za Yesu, japokuwa aliujua ubatizo wa Yohana. Priscilla na Akila ndiyo waliomfundisha usahihi na ukamilifu katika Yesu Kristo. Alipotaka kuendelea na safari yake alipewa ujumbe wa Injili kuupeleka huko Akaya, naye kama kawaida yake alipeleka ujumbe akazidi kuhubiri Injili.

Hitimisho ni Apolo kuwashinda Wayahudi mbele ya watu wote, kwa kufundisha kuwa Yesu ni Kristo. Baada ya kufundishwa juu ya ubatizo wa Yesu mwenyewe kwa Roho Mtakatifu, alizidi kuhubiri kuwa Yesu ni Kristo. Yesu ni Kristo, ambaye hukaa kwetu kwa njia ya neno lake. Tusimuache daima. Amina

Jumatano njema

Heri Buberwa