Date: 
25-02-2025
Reading: 
Waebrania 4:8-13

Jumanne asubuhi tarehe 25.02.2025

Waebrania 4:8-13

8 Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye.

9 Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.

10 Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.

11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi.

12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.

Neno la Mungu ni silaha imara;

Somo la asubuhi ya leo ni mojawapo ya nukuu nzito katika Biblia kuhusu nguvu ya Neno la Mungu. Mwandishi analionya Kanisa la Hebrania kuhusu hatari ya ukristo wa utamaduni. Anasema Neno la Mungu lina nguvu, li hai, lina ukali kuliko upango ukatao kuwili. Katika somo hili naweza kusema "Neno la Mungu" ni ujumbe wake Mungu kupitia kupitia mahubiri na mafunuo mbalimbali kwa njia ya Yesu Kristo kama yalivyotunzwa tangu kale.

Tafsiri ya maandiko huonesha kwamba "Neno" ni Yesu Kristo ambaye Yohana anamuita "Neno" (Yoh 1:1). Mwandishi katika somo la asubuhi ya leo anasema ''maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu..." lakini ukisoma kuanzia nyuma kidogo unaona ambavyo Israeli hawakumsikia Bwana japokuwa ilikuwepo habari njema kwa ajili yao;

Waebrania 3:9-11

9 Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arobaini.
10 Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu;
11 Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu.

Mwandishi anatuasa kutokuwa kama hao waliomuasi Mungu kwa kutolisikia neno lake. Kumbe Neno la Mungu ndiyo msingi wa Kanisa na waaminio kwa ujumla. Ndiyo maana katika ibada, sehemu ya mahubiri huwa ni ya pekee. Tusome, tujifunze na kulisikia Neno la Mungu maana kwa njia hiyo tunamshika Yesu aliyekuwepo tokea mwanzo akatukomboa kwa kufa msalabani. Tumshike yeye aliye Neno la uzima ili tuwe na mwisho mwema. Amina

Jumanne njema

Heri Buberwa