Date: 
22-02-2025
Reading: 
Nehemia 9:18-29

Jumamosi asubuhi tarehe 22.02.2025

Nehemia 9:18-26

18 Naam, hata walipojifanyia ndama ya kusubu, na kusema, Huyu ndiye Mungu wako aliyekupandisha kutoka Misri, tena walipokuwa wamefanya machukizo makuu;

19 hata hivyo wewe kwa wingi wa rehema zako hukuwaacha jangwani; nguzo ya wingu haikuwaondokea wakati wa mchana, ili kuwaongoza njiani; wala nguzo ya moto haikuondoka wakati wa usiku, ili kuwapa mwanga na kuwaonyesha njia watakayoiendea.

20 Ukawapa na roho yako mwema ili kuwaelimisha, wala hukuwanyima mana vinywani mwao, tena ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.

21 Naam, muda wa miaka arobaini uliwaruzuku jangwani, wasihitaji kitu; nguo zao hazikuchakaa, wala miguu yao haikuvimba.

22 Pamoja na hayo ukawapa falme na taifa za watu, ulizowagawia sawasawa na mafungu yao; hivyo wakaimiliki nchi ya Sihoni, naam, nchi yake mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu, mfalme wa Bashani.

23 Watoto wao nao uliwaongeza kama nyota za mbinguni, ukawaingiza katika nchi ile, uliyowaambia baba zao kuwa wataingia kuimiliki.

24 Basi wale watoto wakaingia wakaimiliki nchi, nawe ukawatiisha wenyeji wa nchi mbele yao, ndio Wakanaani, ukawatia mikononi mwao, pamoja na wafalme wao, na watu wa nchi, wawatende kama wapendavyo.

25 Wakaitwaa miji yenye boma, na nchi yenye neema, wakazitamalaki nyumba zilizojaa vitu vyema, birika zilizochimbwa, mizabibu, na mizeituni, na miti mingi yenye matunda; hivyo wakala, wakashiba, wakanenepa, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.

26 Walakini hawakukutii, wakakuasi, wakaitupa sheria yako nyuma yao, wakawaua manabii wako walioshuhudu juu yao wapate kuwarejeza kwako; wakatenda machukizo makuu.

Tunaokolewa kwa neema ya Mungu;

Somo la leo asubuhi hii ni mwendelezo wa somo la juzi asubuhi (Alhamisi) ambapo tuliona kundi lilikusanyika kwa ajili ya toba, Ezra akiwaongoza kufanya toba. Katika somo tulilosoma, Ezra anaendelea kufanya toba akielezea mabaya waliyofanya Israeli. Katika hiyo sala anaeleza jinsi Mungu alivyowaongoza kwa miaka 40 jangwani, akawarehemu na kuendelea kuwapa uzao, pamoja na maovu yao. Pamoja na baraka zote bado hawakuwa watii, ndipo Ezra anawaongoza kufanya toba.

Mstari wa 18 unaonesha kuwa Israeli walifanya machukizo mbele za Mungu, lakini mstari wa 19 unasema kuwa kwa wingi wa rehema zake (Mungu) hakuwaacha jangwani, nguzo ya wingu haikuwaondokea mchana, na nguzo ya moto haikuwaondokea usiku kuwaongoza. Hata sasa neema ya Mungu haikomi, hututunza na kuturehemu katika yote. Tumuishie yeye daima. Amina

Jumamosi njema

Heri Buberwa