Ijumaa asubuhi tarehe 21.02.2025
Kutoka 19:1-8
1 Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai.
2 Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima.
3 Musa akapanda kwa Mungu, na Bwana akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya;
4 Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi.
5 Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu,
6 nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.
7 Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, Bwana aliyokuwa amemwagiza.
8 Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema Bwana tutayatenda. Naye Musa akamwambia Bwana maneno ya hao watu.
Tunaokolewa kwa neema ya Mungu;
Wana wa Israeli walikuwa njiani kuelekea nchi ya ahadi, wakapiga kambi jangwani. Musa anapewa maelekezo na Mungu kwamba walishike agano lake, ndipo watakuwa tunu kwake (Mungu) maana dunia yote ni mali yake. Ni ujumbe uliolenga kuwaambia Israeli kuendelea kumshika Bwana katika safari yao kuelekea Kanani.
Ujumbe wa Mungu kupitia kwa Musa kwenda kwa watu wake ni watu hao kushika agano lake, akiwaahidi kuwa Taifa takatifu. Kama ahadi ya Mungu ilivyo, sisi ni Taifa takatifu kwa sababu tumeokolewa na Yesu kwa njia ya kifo msalabani na kufufuka toka kaburini. Wokovu huu ni bure, kwa neema. Mwamini sasa uokolewe. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa