Date: 
20-02-2025
Reading: 
Nehemia 9:16-17

Alhamisi asubuhi tarehe 20.02.2025

Nehemia 9:16-17

16 Lakini wao na baba zetu wakatakabari, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wala hawakuzisikiliza amri zako,

17 ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha.

Tunaokolewa kwa neema ya Mungu;

Taifa la Mungu lilikuwa limekusanyika kwa toba. Walikusanyika wote na wakati wa sala ukiendelea, Ezra akawaongoza kufanya toba. Somo tulilosoma ni sehemu ya Sala, Ezra akiwaongoza watu kutubu dhambi zao kwa Mungu aliyewakomboa kutoka utumwani.

Taifa la Mungu walitubu dhambi baada ya kufahamu kuwa walikosa, walitenda dhambi. Bila shaka walijua kuwa maisha yao hayakuwa na Utukufu wa Mungu. Waliikimbilia neema ya Mungu, na uamuzi sahihi waliofanya ni kutubu. Uamuzi sahihi kwetu ni kuishi maisha ya toba, ili tuishi maisha yenye kumshuhudia Kristo. Amina

Alhamisi njema

 

Heri Buberwa