Jumatano asubuhi tarehe 19.02.2025
Luka 15:11-32
11 Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili;
12 yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake.
13 Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.
14 Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.
15 Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.
16 Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.
17 Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.
18 Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;
19 sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.
20 Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.
21 Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.
22 Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;
23 mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi;
24 kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.
25 Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo.
26 Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini?
27 Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.
28 Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi.
29 Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;
30 lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.
31 Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.
32 Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.
Tunaokolewa kwa neema ya Mungu;
Leo asubuhi tunasoma juu ya mwana mpotevu aliyeomba urithi wake, baada ya kuuza mali zake akaondoka na kwenda nchi ya mbali. Alitumia vibaya fedha zake kwa starehe na ilifikia hatua akaishiwa. Baada ya kufanya vibarua kadhaa ndipo aliamua kurudi kwa baba yake. Yeye alijifanya mtumwa akiomba kupokelewa, lakini ikawa kinyume chake.
Baba yake alimpokea kwa shangwe kubwa. Aliamuru achinjwe ndama aliyenona, akaamuru avalishwe nguo safi, viatu vipya na pete kidoleni. Baba huyu anatuonesha mfano wa huruma ya Mungu ambaye hutusamehe dhambi zetu bure pale tunapotubu. Haangalii tumefanya nini, huangalia toba yetu. Hii ndiyo neema ya Mungu. Basi na tukae kwa Kristo mwenye kutusamehe daima, hata uzima wa milele. Amina.
Jumatano njema
Heri Buberwa