Jumanne asubuhi tarehe 18.02.2025
Esta 5:1-8
1 Ikawa siku ya tatu Esta alijivika mavazi yake ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuielekea nyumba ya mfalme; naye mfalme akaketi juu ya kiti chake cha enzi katika nyumba ya mfalme, kuuelekea mlango wa nyumba.
2 Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo.
3 Mfalme akamwambia, Malkia Esta, wataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme.
4 Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia.
5 Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyosema. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta.
6 Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa.
7 Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii,
8 Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunifanyizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema.
Tunaokolewa kwa neema ya Mungu;
Habari hii ni sehemu ya jinsi Wayahudi walivyookelwa kuangamizwa, kwa msaada wa Esta. Hamani alitangaza kuangamizwa kwa Wayahudi wote! Mordekai na wenzake wote wakaona hawana maisha tena! Wakamwambia Esta kwamba tusipopona hata wewe hautapona, mwendee mfalme kwa nafasi yako ya umalkia tusiangamizwe.
Ukiendelea kusoma unaona kuwa Esta alifanikisha kutokuangamizwa kwa Wayahudi. Hamani aliyetangaza kuangamiza Wayahudi alikufa kwa kutundikwa mtini. Wengine wakifika hapa husema adui zako watatundikwa mtini! Kumbe sisi tuone Wayahudi walivyokombolewa wasiangamizwe, tukikumbuka tulivyookolewa na neema, na kudumu katika neema hii ya wokovu. Amina
Jumanne njema
Heri Buberwa