Jumatatu asubuhi tarehe 17.02.2025
Mwanzo 41:28-36
28 Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.
29 Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri.
30 Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi.
31 Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana.
32 Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.
33 Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri.
34 Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba.
35 Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji.
36 Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa.
Tunaokolewa kwa neema ya Mungu;
Farao aliota ndoto ambayo alishindwa kujua tafsiri yake. Waganga wote na wanajimu walishindwa kutafsiri ndoto ile. Yusufu aliyekuwa mfungwa akatolewa kutafsiri ndoto ya mfalme. Somo tulilosoma ni sehemu ya maneno ya Yusufu akitafsiri ndoto ya mfalme, kwamba itakuja miaka saba ya shibe na miaka saba ya njaa. Yusufu anaenda mbele zaidi na kumtaka Farao kukusanya chakula cha kutosha wakati wa shibe, ili nchi isikumbwe na njaa miaka saba ya njaa itakapowadia.
Baada ya kuota ndoto, Farao aliwaita waganga na wachawi wote kutafsiri ndoto ile, wakashindwa! Akaletwa Yusufu aliyekuwa na Roho wa Mungu kutafsiri ndoto ya mfalme. Farao alikiri kuwa Yusufu alikuwa na Roho wa Mungu baada ya Yusufu kuitafsiri ndoto;
Mwanzo 41:38-39
38 Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? 39 Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.Siyo wachawi na waganga walioweza kutafsiri ndoto ya Yusufu, bali Yusufu aliyekuwa na Roho wa Mungu. Si kwa nguvu wala uwezo wetu tunaweza lolote, bali tunayaweza yote kwa nguvu ya Mungu ambaye ametuokoa kwa Neema. Amina.
Tunakutakia wiki njema
Heri Buberwa